Kiungo wa JKU azitoa udenda Simba, Yanga

Friday January 12 2018

 

By THOBIAS SEBASTIAN

Zanzibar. KIUNGO fundi wa JKU, Faisal Salum ‘Toto’ ameziweka kati timu za Simba na Yanga ambazo sasa zinahaha kumsajili ambapo tayari zimeulizia mkataba wake na timu hiyo unamalizika lini.

Kiungo huyo fundi wa pasi alimzima kabisa mkali wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi kwenye mchezo wao wa hatua ya makundi ambao Wanajangwani hao walishinda dakika za jioni kwa bao la juhudi binafsi za Hassan Kessy.

Toto alisema baada ya timu yao kuondolewa katika kombe la Mapinduzi viongozi wa vigogo hao wa soka nchini walimfuata kwa nyakati tofauti ili kuzungumza naye.

“Nimezingumza na viongozi wakubwa wa Yanga na Simba ambao sitaweza kuwataja majina yao, lakini walikuwa wanataka kujua mkataba wangu na JKU unamalizika lini,” alisema.

“Tofauti na kuongea uso kwa uso na viongozi hao nimeongea katika simu na viongozi wa Singida United, Azam na Mtibwa Sugar ambao pia nimezungumza nao kuhusu mambo ya usajili na naimani kuwa msimu ujao nitacheza Bara,” alisema Toto.