Kiungo wa Ghana alazwa, kisa damu kuganda mapafuni

Muktasari:

Badu atabaki hospitalini kwa siku kadhaa kwa ajili ya uangalizi zaidi. Staa huyo yupo kwa mkopo kwenye kikosi hicho cha Hellas Verona, huku ikiwa na uwezekano wa kumsajili jumla kutoka Udinese.

MILAN, ITALIA . KIUNGO wa kimataifa wa Ghana, Emmanuel Agyemang Badu amekimbizwa hospitali huko Italia baada ya kugundulika kuwa ana tatizo la damu kuganda kwenye mapafu.

Klabu yake ya Hellas Verona inayokipiga kwenye Serie A, imetoa taarifa Jumanne iliyopita kwamba kiungo wao huyo amelazimika kupelekwa hospitali baada ya kupata tatizo la kupumua.

Staa huyo wa Black Stars mwenyewe alisema jana Alhamisi kwamba kwa sasa anaendelea vizuri.

Badu atabaki hospitalini kwa siku kadhaa kwa ajili ya uangalizi zaidi. Staa huyo yupo kwa mkopo kwenye kikosi hicho cha Hellas Verona, huku ikiwa na uwezekano wa kumsajili jumla kutoka Udinese.

Hakuwamo kwenye kikosi cha Ghana kilichocheza michuano ya Afcon 2019 huko Misri kwa sababu tu alirudi uwanjani Machi mwaka huu baada ya kuwa majeraha kwa miezi 11.