Kiungo mpya: Hata aje nani, naanza Yanga

IKIWA hata dirisha la usajili halijafunguliwa wala Ligi Kuu kumalizika, tayari jina la kiungo matata anayekipiga Tanzania Prisons, Cleophas Mkandala limeanza kuumiza vichwa vya mabosi wa timu ya soka ya Yanga.

Mkandala ambaye aliwahi kukaa kwa Wanajangawani hao kwenye timu ya vijana (U-20), kwa sasa amekuwa gumzo huku Azam FC wakitoa jasho kupata saini yake kwa ajili ya msimu ujao.

Hadi sasa Ligi Kuu imesaliwa na michezo takribani 10 kwa baadhi ya timu, huku nyingine zikiwa na tisa kumaliza msimu ambapo Simba, Yanga na Azam FC zimeshaingia mawindoni kusaka nyota wapya. Mkandala ambaye ni msimu wake wa tatu kucheza Ligi Kuu akiwa na Wajelajela hao wa jijini Mbeya, amekuwa katika kiwango bora na kuzifanya timu hizo kongwe kushawishika kumchukua.

Katika makala haya, kiungo huyo ameeleza kwa mapana jinsi alivyojiandaa kutua tena Yanga kukabiliana na changamoto ambazo awali zilimtimua pamoja na malengo yake kwenye soka.

Ligi za chini

Mkandala anasema moja ya vitu anavyojivunia kwenye maisha ya mpira hadi sasa ni kutocheza ligi za chini kwani baada ya kuipandisha Ukonga Rangers katika ngazi ya Mkoa wa Dar es Salaam hajarudi tena huko.

Anasema baada ya kumalizika kwa msimu huo aliingia kwenye mchujo katika Klabu ya Yanga kujaribu bahati na kati ya wachezaji 400 waliojitokeza jina lake lilikuwa la kwanza.

Anasema licha ya kutodumu na Yanga katika kikosi cha vijana, alihitaji kuonyesha uwezo wake japokuwa alifanyiwa fitina na waliokuwa kwenye benchi la ufundi.

“Nilicheza Daraja la Nne kule Dar es Salaam katika timu ya Ukonga Rangers nilikoipandisha ngazi ya mkoa, nikaenda majaribio Yanga nikafuzu japo maisha ya pale yalinipa huzuni,” anasema Mkandala.

Kilichomkimbiza Yanga

Kiungo huyo mwenye kasi uwanjani anasema alihitaji kuendelea kuwapo Yanga, lakini alikatishwa tamaa na waliokuwa makocha Shadrack Nsajigwa na Anthony Kibasa ndipo aliamua kuondoka.

Anasema katika mashindano ya ligi ya vijana mwaka juzi yaliyofanyika mkoani Kagera hakupata nafasi katika michezo yote saba na muda mwingine hata benchi hakuwapo.

Mchezaji huyo anasema ilifikia hatua kikapangwa kikosi, lakini jezi yake ilibaki nje na kushuhudia baadhi ya mechi akiwa jukwaani.

“Unajua sisi kituo chetu kilikuwa Kagera, lakini niliishia benchi na jukwaani na baadaye nikaambiwa tukifika Dar es Salaam nitaachwa, kwa hiyo kwa kuangalia zile changamoto nikaona niondoke nisake maisha mapya,” anasema mchezaji huyo.

Anaongeza kuwa baada ya kutoka Yanga alirudi jijini Mbeya kwenye mashindano ya ndondo yajulikanayo kama Mastara Cup ambapo aliweza kuonyesha uwezo mkubwa na kunyatiwa na timu nyingi.

Anasema kuwa msimu huo wa 2017/18 baada ya kumalizika kwa michuano hiyo, timu za Mbeya City, Njombe Mji na Lipuli zilizokuwa zimepanda Ligi Kuu na Prisons zilimhitaji.

Mchezaji huyo anasema pamoja na ofa hizo aliamua kukaa na kutulia ili kutokurupuka kujiunga na timu yoyote na kuamua kumwaga wino klabuni Tanzania Prisons ambapo hadi sasa anatesa.

“Timu nyingi zilikuja kweli kama Lipuli, Njombe Mji, Mbeya City lakini niliamua kwenda Prisons ambao niliamini nitafanya nao kazi na ninashukuru naendelea vizuri.”.

Anasema tangu alipojiunga na Maafande hao hajutii kwani ilikuwa iwe ni maslahi na ushirikiano kikosini hakuna penye tatizo na kwamba, wakiamua jambo wanashirikishana wachezaji wote.

Anasema uwapo wa wachezaji wenye uwezo na uzoefu kama Raulian Mpalile, Salum Kimenya, Fredy Chudu na wengine umempa kujiamini awapo uwanjani na amejifunza mengi kutoka kwao.

“Maisha ya Prisons yamekuwa mazuri sana, siwezi kujutia hata siku moja kuanzia ndani hadi nje ya uwanja na nimependelea zaidi kuwa na wachezaji kama Kimenya, Chudu, Mpalile na wengine,” anasema Mkandala.

Hata hivyo, anaeleza kwamba anachofurahia kwa muda wote aliotumikia timu hiyo, ni kuwa haijawahi kushuka daraja na badala yake imekuwa katika ubora kwa misimu yote.

Anarudi hivi Yanga

Mkandala anaweka wazi kuwa pamoja na kwamba Yanga ni timu kubwa na kongwe, lakini anaijua vizuri na kwamba iwapo mazungumzo yatamalizika vyema hana wasiwasi na namba.

Anasema kuwa awali hakuwa na uzoefu wowote kwenye timu hiyo, lakini amejiandaa vyema kisaikolojia na kiushindani muda utakapofika wa kuungana nao msimu ujao.

Anaeleza kwamba kutokana na uwezo wake ulivyo miguuni hana presha kubwa kwani atakuwa makini kusikiliza na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi kwa kuwa malengo yake ni kufika mbali.

“Niko tayari kurudi Yanga, sina wasiwasi kwenye ishu ya namba kwa sababu najiamini uwezo wangu, (Yanga) ni timu kubwa naiheshimu ndio maana najiandaa kila namna ili mambo yakikaa sawa nisipate tatizo.”

“Nilipoondoka (Yanga) kwanza nilikuwa bado sijacheza soka la ushindani, lakini kwa sasa naamini kitamvutia kila mmoja, kifupi nimejipanga.”

Ashtukia jambo

Anasema ni kama akitua Yanga msimu ujao, hali haitakuwa ya kawaida kwenye vita ya namba kutokana na ushindani utakaokuwapo.

Anasema anasikia usajili wa timu hiyo namna unavyokwenda, jambo ambalo linamfanya kuendelea kujifua zaidi kukabiliana na nyota kutoka ndani na nje ya nchi na kwamba anasubiri muda ufike.

Mkandala anaongeza kuwa licha ya kwamba mashabiki na wadau wa soka nchini wamekuwa wakiwaamini zaidi ‘maproo’ lakini kwa tizi analopiga anaamini watakubali mziki wake.

Anasema hata wakisajiliwa nyota wa kimataifa 100 lakini kwa soka alilo nalo uhakika wa namba Yanga uko palepale kutokana na jinsi anavyofanya klabuni Prisons.

“Unajua mashabiki wengi hapa nchini wanawapa sana sifa wachezaji wa nje, lakini naamini kwa uwezo wangu nikitua Yanga watanikubali kwa sababu ushindani hata hapa Prisons upo.”

Anaongeza kuwa kinachompa kujiamini zaidi ni uwezo wa kucheza namba nne tofauti ikiwa ni winga zote na nafasi mbili za mbele (8 na 10) na kwamba, kuna muda hucheza hata namba sita.

Meneja amaliza kazi

Meneja wa mchezaji huyo (jina tunalo) anasema malengo yake ni kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, hivyo licha ya kuwapo kwa ofa nyingi lakini lazima akipige Yanga.

Anasema hadi sasa Azam FC imeshaonyesha nia ya kuhitaji huduma ya kiungo huyo, lakini wamekaa na kutafakari ili wasikwame huko mbeleni lazima wafanye uamuzi mgumu.

Anasema mara kadhaa wachezaji wanaotoka timu za Simba na Yanga wamekuwa na urahisi wanapokweda kwenye timu za kimataifa kutokana na rekodi zao, hivyo wanasubiri muda.

“Azam nao wanahitaji huduma yake, lakini nataka Mkandala afikie malengo yake na nimeona bora acheze Yanga ili apate changamoto mpya,” anasema meneja huyo aliyesisitiza kuwa hataki kutajwa jina lake.

Anasema kuwa kabla ya janga la ugonjwa wa corona kutikisa duniani, walipata ofa kutoka timu ya St Luis ya Shelisheli na kila kitu kilikuwa tayari, lakini gonjwa hilo liliharibu mipango.