Kiungo afichua kinachoimaliza Mtibwa Sugar

Muktasari:

Mtibwa inashika nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 37

Kiungo wa Mtibwa Sugar, Mtibwa Sugar Awadhi Juma amesema kuwa kufanya vibaya kwa timu hiyo msimu huu kumesababishwa na ushindani uliopo kwenye Ligi Kuu na sio vinginevyo.

Mtibwa Sugar ni miongoni mwa timu zilizo kwenye hatari ya kushuka daraja ikiwa imevuna pointi 37 hadi sasa huku ikiwa nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu.

Akizungumza na Mwanaspoti, kiungo huyo alisema kuwa idadi kubwa ya timu zimeonesha kuimarika msimu huu jambo linalofanya iwe ngumu na yenye ushindani.

“Hakuna mchezaji ambaye anaingia uwanjani akatamani timu yake ifungwe hapana, inakuwa ni sehemu tu ya matokeo ambayo yanatokea.

Huu msimu umekuwa na ushindani mkubwa sana na ndio maana timu nyingi zinazidiana pointi chache,” alisema kiungo huyo.

Anasema, watahakikisha mechi zilizosalia wanashinda na timu yao inasalia katika ligi kuu, kwa kuwa nia na uwezo wanao licha ya ushindani mkubwa uliopo.

Nyota huyo wa zamani wa Simba alisema kuwa wachezaji wa Mtibwa Sugar hawafurahishwi na mwenendo wa kusuasua wa timu yao kwenye ligi kwani sio jambo ambalo wamelizoea.