Kiungo Yanga, Ally Yusuf ‘Tigana’ amefariki dunia leo

Muktasari:

Uongozi wa klabu ya Yanga umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha mchezaji wetu wa zamani Ally Yusuf ‘Tigana’ kilichotokea leo mchana.

Dar es Salaam. Kiungo wa zamani wa Yanga, Ally Yusuf ‘Tigana’ amefariki dunia leo Alhamis mchana katika hospitali ya Amana, Jijini Dar es Salaam baada ya kuugua ghafla na kukimbizwa hospitali hapo.

Akithibisha kifo hicho, mchezaji Lubigisa Lubigisa alisema ni kweli Tigana amefariki leo mchana baada ya kuugua ghafla kuhara na kutapiki na kukimbizwa hospitali ya Amana ambako mauti yamemkuta.

Lubigisa alisema awali mke wa Tigana ndio alikuwa akiumwa na alikuwa amelazwa Amana, hivyo jana Jumatano alipokwenda kumuangalia hali ya mchezaji huyo ikaanza kubadilika.

"Alipofika nyumbani hali yake ikabadilika, akaanza kutapika na kuharisha kisha kukimbizwa hospitalini Amana, lakini baada ya kufika hapo alizidi kubadilika zaidi kutokana na kutapika akazidi kuishiwa nguvu," alisema Lubuigisa.

Aliongeza kutokana na hali alizidi kupungua hadi mauti yalipomkuta mchezaji huyo.

Uongozi wa Yanga kupitia ukurasa wake wa Instagram umetoa pole kwa familia ya Tigana kwa kuandika. Uongozi wa klabu ya Yanga umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha mchezaji wetu wa zamani Ally Yusuf ‘Tigana’ kilichotokea leo mchana.

Tigana aliichezea Yanga kwa vipindi viwili aliingia 1994-1995 na baadaye 2001-2004. Mungu ailaze roho ya maheremu mahali pema peponi amini.’

Tigana amekulia Ilala na kwenye Timu ya Yosso FC iliyokuwa chini ya kocha Elias Nyika ambayo alikuwa anafanya mazoezi na kucheza michezo ya kirafiki pamoja na kucheza ligi mbalimbali na hatimaye ikabadilishwa jina ikaitwa Shauri Moyo Combine na badaye kubadilishwa tena jina na kuitwa Shauri Moyo Kids hadi ilipopanda Ligi Daraja la Nne.

Mwaka 1989 baada ya kupandisha Timu ya Shauri Moyo Kids akapata nafasi ya kujinga na Manyema FC ambayo ilikuwa ikicheza Ligi Daraja la Tatu kwa ushawishi wa Juma Mensa.

Msimu wa mwaka 1990/91 ilijisalimisha Pan African kwa mkataba mpya akilamba kitita cha Sh500,000 kipindi hicho bosi wa Pan alikuea Murtaza Dewji ambapo kambi ilikuwa Tazara

Kocha wa Timu ya Taifa Sunday Kayun enzi hizo alifurahishwa na kiwango chake, bila kujali umbile lake kuwa dogo, akamjumuisha kwenye kikosi kilichokuwa kinajiandaa na Michuano ya Chalenji ambayo yalikuwa yafanyike Nchini Kenya mwaka 1991.

Baada ya kuwasumbua Yanga kwenye michezo ya Ligi Daraja la Kwanza (Ligi Kuu) kipindi hicho ikiwa kwenye kiwango kikubwa matajiri wa Yanga wakiongozwa na Abass Gulamali wakamfungia kazi kuhakikisha wanampata

Simba Watoa Dau Nene

Baada ya kufukuziwa na Simba kwa muda wa zaidi ya miaka mitano bila ya mafanikio ndipo, Tigana alipoingia kwenye rada za wanamsimbazi mwaka 1995 kwa dau la Sh1,500,000 klabu aliyoitumikia kwa muda wa miaka miwili kisha kutimukia Mauritius kwenye Timu ya Skauti SC iliyokuwa ikishiriki ligi kuu kwa misimu miwili

 

Sababu kubwa illiyosababisa aondoke Yanga ni kutokana na klabu hiyo kuyumba kiuchumi huku wachezaji wengi wazuri kuondoka, wengine wakienda Malindi, Simba na Tukuyu.

Baada ya kutoka Mauritius aliweza kuzitumikia Klabu za Simba na Yanga kwa nyakati Tofauti kabla ya kuzinguana na Bosi wa Simba Azim Dewji kwa kumtuhumu kuuza mchezo dhidi ya Yanga uliochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha ambapo Yanga ilishinda bao 2-1

Akaona isiwe taabu maana umri nao ukawa unamtupa mkono akaenda Moro united (Chelsea ya Bongo) ambayo walilifanikiwa kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara na mkataba ulipoisha akaenda zake Afrika kusini kusaka timu ila hakufanikiwa ndipo akaanza kusomea ukocha na timu yake ya kwanza kuifundisha ilikuwa  Friend Rangers ikiwa Ligi daraja la Kwanza (FDL) na baadaye JKT Oljoro.