Kiungo Sneijder ameamua kustaafu soka

Tuesday August 13 2019

 

AMSTERDAM, Uholanzi. Nyota wa zamani wa Real Madrid, Inter Milan na Uholanzi, Wesley Sneijder ametundika daluga baada ya kulitumikia soka kwa miaka 17.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 alicheza mechi 134 kwa nchi yake na alikuwepo katika kikosi kilichoshiriki fainali za Kombe la Dunia 2010.

Katika maisha yake ya soka, alitwaa ubingwa wa La Liga akiwa na Real Madrid pia akanyanyua Kombe la Serie A, Ligi ya Mabingwa na Coppa Italia mara tatu akiwa na Inter Milan mwaka 2009-10.

Sneijder atapewa nafasi mpya katika klabu ya nyumbani kwao FC Utrecht.

“Kwa sasa nimestaafu soka, nataka sehemu nzuri ya kukumbukia mambo yangu na kutoa msaada wangu,” alisema.

Mchezaji huyo ni zao la Shule ya Soka ya Ajax na alitua  Real Madrid  mwaka 2007 kwa ada ya Pauni 23 milioni.

Advertisement

Maisha yake ya soka Ulaya yalimpa nafasi ya kucheza Galatasaray ya Uturuki, Nice ya Ufaransa kabla ya kutimkia Al Gharafa ya Qatar.

Katika timu ya taifa, Sneijder alifanikiwa kumaliza nafasi ya pili katika Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini baada ya Uholanzi kufungwa na Hispania katika fainali.

Advertisement