Kiungo Simba atua Uarabuni

Muktasari:

Shiboub ameitumikia Simba kwa msimu mmoja ambao ameifungia   mabao manne na kupiga pasi sita za mwisho.

Kiungo wa zamani wa Simba, Sharaf Eldin Shiboub leo Oktoba 24, 2020 ametambulishwa rasmi na timu ya CS Constantine inayoshiriki Ligi Kuu ya Algeria baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili.

Shiboub mwenye umri wa miaka 26, amejiunga na Constatine akiwa mchezaji huru mara baada ya kutoongezewa mkataba na Simba katika dirisha kubwa la usajili miezi miwili iliyopita.

Taarifa iliyotolewa na klabu ya CS Constantine imeeleza kuwa Shiboub anayechezea timu ya taifa ya Sudan, amejiunga nao sambamba na nyota mwingine Mohamed Bin Taher.

"Leo, wachezaji Mohamed bin Taher na nyota wa kimataifa wa Sudan, Sharaf Eldin  Shiboub wamejiunga na klabu ya Constantine ambayo wataitumikia kwa mikataba ya miaka miwili.

Wachezaji hao wapya walisaini mikataba ya awali na Constantine lakini hawakuweza kuwasili Algeria kutokana na tatizo la virusi vya Corona.

Hata hivyo uongozi wa timu umefanya kila liwezekanalo kuhakikisha wachezaji hao wanaungana na timu," ilisema taarifa ya klabu hiyo.

Shiboub akiwa na Simba, licha ya kutopata nafasi ya kutosha ya kucheza msimu uliopita, alifunga jumla ya mabao manne na kupiga pasi sita za mwisho.