Kiungo Prisons ajifunga Stand

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Kassim alisema wamemalizana na Stand na tayari ameungana na timu hiyo ili kuitumikia kupitia dirisha dogo ila mipango yake ni kutimkia nje ya nchi kucheza soka la kulipwa.

KIUNGO wa zamani wa Prisons, Kassim Khamis amesaini mkataba wa miezi sita kuitumikia Stand United na kuweka bayana amefanya hivyo kwa nia ya kujiweka fiti kabla ya kutimka nje ya nchi mwakani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kassim alisema wamemalizana na Stand na tayari ameungana na timu hiyo ili kuitumikia kupitia dirisha dogo ila mipango yake ni kutimkia nje ya nchi kucheza soka la kulipwa.

Alisema hayupo tayari kuweka wazi ni timu gani inayomuhitaji nje ya nchi kikubwa anachoweza kuzungumzia ni Stand aliyojiunga nayo kwa lengo la kuisaidia iweze kufanya vizuri zaidi ya hapo ilipo sasa.

“Nimeingia mkataba wa miezi sita kwa vile hili ni dirisha dogo la usajili sitakiwi kujifunga muda mrefu najitengenezea mazingira ya kutoka nikiwa huru bila kubanwa, tayari nina mazungumzo na timu nyingine kutoka nje ya nchi,” alisema Kassim.

Khamis aliongeza Stand ni timu kubwa inaweza ikampa changamoto na kumrudisha katika nafasi yake baada ya kupotea kutokana na majeraha.