Kiungo Mbamba: Nimekuja kuipigania bendera ya Kenya, siyo kuuza sura

Muktasari:

  • Harambee Stars ipo Kundi C, pamoja Tanzania,  Algeria na Senegal, itaanza kutupa karata yake Juni 23, dhidi ya Algeria, kisha itavaana na Tanzania (Juni 27) kabla ya kumalizana na Senegal,  Julai mosi.

Nairobi.  Timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars itakapojitosa uwanjani katika fainali ya AFCON huko Cairo Misri, wachezaji 23 watakuwa na uhakika wa kuipigania bendera ya taifa, akiwemo kiungo mshambuliaji Christopher Mbamba.

Ikiwa ni mara yake ya kwanza kuwakilisha Kenya katika soka la kimataifa, Mbamba mzaliwa wa Zimbabwe, akiwa na asili ya Kenya kwa upande wa Mama na Namibia kwa upande wa baba, amesititiza kuwa Kocha mkuu wa Stars, Sebastien Migne alimuita kucheza soka na sio kuuza sura, jukumu ambalo yuko tayari kutekeleza.

Mbamba amewahi kuwachezea timu ya taifa ya vijana ya Sweden, alisema licha ya Sweden kumbembeleza awakilishe taifa, kwa muda mrefu amekuwa na ndoto ya kuvaa jezi ya timu ya taifa ya Kenya ndio maana, Machi mwaka huu, alipoitwa hakusita kukubali wito.

“Ni ndoto ya kila mchezaji kuchezea timu ya taifa. Niliichezea Sweden ya vijana, lakini akili yangu ilikuwa inaiwaza Kenya. Nilipopata fursa sikujiuliza mara mbili. Nafahamu ushindani ni mkubwa ila nimejipanga," alisema.

Mbamba ni sehemu ya nyota 27 wa Stars waliokita kambi nchini Ufaransa kujiandaa na fainali za AFCON zitakazotimua vumbi kuanzia Juni 21 hadi Julai 19, nchini Misri.

Kenya inayoshiriki michuano hii kwa mara ya kwanza baada ya kuzikosa kwa zaidi ya miaka 15, itacheza mechi mbili za kirafiki ya kwanza, ikiwa ni dhidi ya Madagascar (Juni 7) na ya pili ikiwa ni dhidi ya DR Congo, itakayopigwa Juni 15, Jijini Madrid.

Harambee Stars ipo Kundi C, pamoja na majirani zao Taifa Stars (Tanzania),  Algeria na Senegal, itaanza kutupa karata yake Juni 23, dhidi ya Algeria, kisha itavaana na Tanzania (Juni 27) kabla ya kumalizana na Senegal,  Julai mosi. Mechi zote zitapigwa Cairo, kwenye Uwanja wa June 30.