Kitenge, Sabilo kummaliza mnyama Taifa

Muktasari:

Simba itawavaa Stand United katika mpambano wa Ligi Kuu na msimu uliopita timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3 kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa.

WAKATI Stand United leo Jumapili inaivaa Simba, benchi la ufundi la klabu hiyo limewapa jukumu zito washambuliaji wake, Alex Kitenge na Sixtus Sabilo kuhakikisha mnyama anakufa mapema kwenye mpambano huo.

Simba itawavaa Stand United katika mpambano wa Ligi Kuu na msimu uliopita timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3 kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa.

Mpaka sasa Simba wana pointi 14 wakiwa katika nafasi ya tano huku Stand United na alama 11 wakishika nafasi ya 11jambo ambalo litafanya mchezo huo kuwa mgumu kwa timu hizo mbili.

Kocha Msaidizi wa Stand United,Athumani Bilali ‘Bilo’ alisema katika kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mpambano huo wamewapa jukumu washambuliaji Kitenge na Sabilo kuhakikisha wanapata mabao ya kutosha.

“Tumejifua vya kutosha kikubwa tunahitaji ushindi hivyo tumewapa jukumu nzito washambuliaji wetu Kitenge na Sabilo la kuhakikisha tunapata mabao mapema na tumewaambia tunawategemea sana,” alisema Bilo.

Alisema watakuwa makini sana kwenye mchezo huo kwani wanakutana na timu bora yenye wachezaji wazuri hivyo ni lazima wacheze kwa uangalifu mkubwa.

“Huu mchezo utakuwa mgumu kwetu na tushawaambia wachezaji wetu kuwa makini tunakwenda kucheza na Simba ambayo ina nyota bora Ligi Kuu hivyo tunahitaji kujituma zaidi uwanjani kama tunataka kushinda”alisema Kocha huyo.