Kitawaka Ulaya utamu wa Ligi ya Mabingwa umerudi

Muktasari:

Kuhusu mchezo wa Dortmund na PSG, wenyeji wa huko Ujerumani hawatakuwa na huduma ya Marco Reus na Thomas Delaney kutokana na kuwa majeruhi, huku wakitarajia pia kukosa huduma ya Julian Brandt. Kocha Favre anaweza kufikiria kutumia fomesheni ya 3-4-3, akitarajia kuwaweka kwenye fowadi yake mastaa Thorgan Hazard, Sancho na Haaland.

MADRID, HISPANIA . HABARI ndio hiyo. Ule utamu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya mtoano ndio huo umewadia mwanangu. Mabingwa watetezi, Liverpool ikiwa kwenye ubora wake itasafiri kuifuata Atletico Madrid katika mchezo wake wa kwanza wa hatua hiyo ya 16 bora utakaopigwa leo Jumanne. Liverpool itarudi uwanjani Wanda Metropolitano miezi kadhaa tangu ilipobeba ubingwa kwa kuwachapa Waingereza wenzao, Tottenham Hotspur.

Macho na masikio ya wengine yatakuwa huko Signal Iduna Park kuwashuhudia wenyewe Borussia Dortmund wenye huduma moto kabisa ya mastaa kama Jadon Sancho na Erling Haaland wakawakabili matajiri wa Ufaransa, Paris Saint-Germain, ambao kikosi chao kimesheheni mastaa wa nguvu akiwamo Neymar, Kylian Mbappe na Mauro Icardi, ambao wanatengeneza fowadi ya mabingwa hao kwa sasa. Mechi ya marudiano itapigwa Machi 11.

Wakiwa wameshinda mara moja tu katika mechi saba za michuano yote, Atletico wataingia uwanjani hii leo wakiwa sio tishio, kuwakabili mabingwa wa Ulaya, Liverpool waliopo kwenye ubora wao. Ndani mwaka 2020 uingie, Diego Simeone na kikosi chake mambo yamekuwa magumu ataingia kuikabili Liverpool ambao kwa msimu huu si timu unayopenda kabisa kukutana nayo. Kwenye mchezo huo, Atletico itakosa huduma ya washambuliaji wake Diego Costa na Joao Felix ambao ni majeruhi huku kukiwa na hatihati pia juu ya beki wao, Kieran Trippier. Liverpool chini ya Jurgen Klopp watakuwa na kikosi chao chote kizima, ambacho kitakuwa na kazi moja tu ya kugawa dozi. Mchezo huo wa leo utakuwa mara ya tano kwa timu hizo kukutana, huku mara zao nyingi walikutana kwenye michuano ya Europa League.

Kuhusu mchezo wa Dortmund na PSG, wenyeji wa huko Ujerumani hawatakuwa na huduma ya Marco Reus na Thomas Delaney kutokana na kuwa majeruhi, huku wakitarajia pia kukosa huduma ya Julian Brandt. Kocha Favre anaweza kufikiria kutumia fomesheni ya 3-4-3, akitarajia kuwaweka kwenye fowadi yake mastaa Thorgan Hazard, Sancho na Haaland.

Mbappe na Icardi ni wachezaji wanaotarajia kuanza kwenye fowadi, huku Angel Di Maria akitarajia pia kuanza kwenye kikosi hicho cha Kocha Thomas Tuchel ambacho amekuwa akipendelea zaidi kutumia fomesheni ya 4-4-2.

Michezo mingine ya hatua hiyo ya mtoano kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya itapigwa kesho Jumatano, ambapo huko Italia, Atalanta watajimwaga uwanjani kwao kuwakabili Valencia, wakati Jose Mourinho na chama lake la Tottenham Hotspur watakuwa London kuwakaribisha Wajerumani, RB Leipzig. Spurs wanasaka nafasi ya kupambana kurudi tena fainali, ambapo msimu uliopita walichapwa na Liverpool kipindi hicho walipokuwa chini ya kocha Mauricio Pochettino.