Kitambi : Wachezaji wa Simba SC morali imeshuka

Muktasari:

Kocha Aussems amesimamishwa kwa muda na uongozi wa Simba jambo lililomfanya Mbelgiji ashindwe kufanya mazoezi na timu hiyo kwa siku tatu.

Dar es Salaam.Kocha msaidizi wa Simba, Denis Kitambi amesema morali ya wachezaji wake ipo chini kutokana na kutokujua hatma ya kocha Patrick Aussems.

Kocha Aussems amesimamishwa kwa muda na uongozi wa Simba jambo lililomfanya Mbelgiji ashindwe kufanya mazoezi na timu hiyo kwa siku tatu.

"Kuhusu morali kweli ipo chini hata wachezaji wanaonekana kuwa na maswali ya hapa na pale na hata nyuso zao kuinamisha chini yote ni kukosekana kwa kocha mkuu," alisema Kitambi.

"Kuhusu kucheza mechi za kirafiki hilo bado sijambiwa na uongozi wangu kwangu nimepewa muda wa wiki moja kuiongoza timu," alisema kocha huyo.

"Lakini hata kuwepo na mchezo wa ligi bado hatujapata taarifa yoyote kutoka kwa bodi ya ligi ingawa bado timu inaendelea na mazoezi kama kawaida kila siku asubuhi," alisema Kitambi.

Katika mazoezi ya leo asubuhi Kitambi aliwafundisha wachezaji wake namna ya kutumia mbinu za kufunga, pia kuhakikisha wanajilinda.

Kitambi aliwapanga mabeki Pascal Wawa, Yusuph Mlipili, Haruna Shamte, Mohammed Hussein 'Tshabalala' na Gerson Fraga.

Wachezaji hawa jukumu lao lilikuwa kukaba na kuwazuia washambuliaji wasiweze kufunga mabao.

Washambuliaji walikuwa Cletous Chama, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu, Said Ndemla na Mzamiru Yassin jukumu lao lilikuwa kufunga tu.

Kitambi alionekana kuwa mkali kwa wachezaji ambao walishindwa kutimiza majukumu yao na kukosa umakini.