Kitaeleweka tu

Muktasari:

Uvumi huo wa kwamba Maguire anakaribia kutua Man United umezua mjadala mkubwa wa namna ambavyo mashabiki wa timu hiyo watapenda timu yao icheze na vile ambavyo hawataki kabisa iwe.

MANCHESTER, ENGLAND.OLE Gunnar Solskjaer amewaambia mabosi wa Manchester United kuchangamka sasa kunasa huduma ya beki Harry Maguire, kwa sababu hawezi kufanya zaidi ya alichokifanya kwa sasa.

Beki huyo ameripotiwa kuiambia klabu yake ya Leicester City isiweke ngumu juu ya suala la kumuuza kama kutakuwa na timu inayoonyesha dhamira ya kufanya hivyo. Man United wanahitaji huduma ya beki huyo wa kati Mwingereza.

Na kinachoelezwa kwa sasa ni kwamba Maguire amebakiza mambo machache sana kukamilisha dili la kutua huko Old Trafford kwa ada ya Pauni 80 milioni, kwa mujibu wa SunSport.

Kama dili hilo likikamilika, Maguire atakuwa beki ghali zaidi duniani akipiku ada ya Pauni 75 milioni iliyolipwa na Liverpool kunasa huduma ya Mdachi Virgil van Dijk kutoka Southampton kwenye dirisha la Januari mwaka jana.

Usajili wa Maguire utazidi kuimarisha beki ya Man United baada ya hivi karibuni kutoa Pauni 50 milioni kunasa huduma ya Aaron Wan-Bissaka, ambaye atakwenda kucheza beki ya kulia huko Old Trafford akitokea Crystal Palace.

Uvumi huo wa kwamba Maguire anakaribia kutua Man United umezua mjadala mkubwa wa namna ambavyo mashabiki wa timu hiyo watapenda timu yao icheze na vile ambavyo hawataki kabisa iwe.

Mashabiki wa wababe hao wa Old Trafford wametumia kurasa zao za mitandao ya kijamii, kujaribu kutengeneza vikosi ambavyo watapenda kicheze kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England, ambapo Man United watakipiga dhidi ya Chelsea.

Lakini, wametengeneza kikosi kingine ambacho watapenda kicheze kwenye mechi za kuzikabili timu zenye fowadi kali kama Manchester City na Liverpool huko kwenye Ligi Kuu England.

Mashabiki hao wametengeneza kikosi ambacho hawatapenda kabisa kocha Solskjaer ajaribu kukianzisha kwenye beki hiyo, kwa sababu wanachoamini kitakuwa majanga tu.

Mechi ya ufunguzi

Kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu England msimu wa 2019/20 dhidi ya Chelsea, mashabiki hao wamechora kikosi chao ambacho watapenda kicheze ambapo kitamhusisha Maguire atakapotua.

Katika mchezo huo utakaopigwa Agosti 11, mashabiki hao kwenye beki wanataka Wan-Bissaka acheza kulia, Luke Shaw beki ya kushoto na kati wasimame Victor Lindelof na Maguire.

Wakicheza fomesheni ya 4-2-3-1, kwenye kiungo wanataka Paul Pogba acheze na Nemanja Matic na kwenye ile safu ya wachezaji watatu nyuma ya mshambuliaji wa kati, Marcus Rashford wacheze Daniel James upande wa kushoto, Anthony Martial kulia na Jesse Lingard katikati kwenye namba 10.

Mashabiki wanaamini kikosi kikianza hivyo kitakuwa na afya ya kuwakabili Chelsea katika mechi hiyo ya mwanzo ya msimu wa Ligi Kuu England na kuanza vyema katika kampeni yao ya kuhakikisha wanafanya vizuri msimu huu.

Mechi dhidi ya Man City

Taarifa za usajili wa Maguire kukaribia zimewapa matumaini makubwa mashabiki wa Man United na kuamini kwamba sasa watakuwa na uwezo wa kutengeneza timu itakayokuwa na nguvu ya kupambana na timu ngumu kama Manchester City na Liverpool msimu unaokuja.

Hata hivyo, mashabiki hao wamechora kikosi na fomesheni ambayo itatosha kuzikabili timu zinazoshambulia muda wote, wakimtaka kocha Solskjaer aanze na mabeki watano kwenye mechi za aina hiyo.

Mashabiki hao wanamtaka Ole atumie fomesheni ya 5-3-2 kwenye mechi kama hiyo ya kuikabili Man City, ambapo anakuwa na mabeki watatu wa kati Maguire, Lindelof na Eric Baily.

Huku Shaw na Wan-Bissaka wakitumika kama mawing-back kushoto na kulia.

Pale kati, safu ya viungo watatu inakuwa na wachezaji Matic, Pogba na Lingard, huku kwenye fowadi ni Martial na Rashford.

Kwenye machaguo yote ya mashabiki kuhusu namna ya timu yao icheze, straika Romelu Lukaku anaonekana kuwekwa kando kabisa pamoja na Alexis Sanchez.

Hilo linatoa ishara kwamba mastaa hao wawili watakuwa na wakati mgumu kwa msimu la kama wataonyesha viwango tofauti kiasi cha kushinikiza kupata nafasi ya kuanza.

Hiki kikosi hakitakiwi

Kocha Solskjaer ameambiwa afanye chochote anachokitaka, lakini asithubutu kupanga kikosi kitakachokuwa na wachezaji kama Phil Jones, Chris Smalling, Diogo Dalot na Ashley Young kwenye safu ya mabeki, hapo atakuwa amefungwa yeye.

Mashabiki hao walichora kikosi ambacho hawataki kabisa kuona beki ikipangwa hivyo, ambapo ni Jones, Smalling, Dalot na Young.

Wanachoamini mashabiki kikosi chenye beki kama hiyo hakiwezi kushinda aina yoyote ya mechi hata kama kwenye fowadi yao na kiungo kutakuwa na wachezaji wenye uwezo kiasi gani.