Kiswahili champeleka darasani bosi mpya Simba

Muktasari:

Klabu ya Simba imemtambulisha Afisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa    anayeingia kuchukua majukumu yaliyoachwa na Crecsentius Magori ambaye ameaga rasmi.

AFISA Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amesema, anakwenda kujifunza Lugha ya Kiswahili ili kuifanya kazi yake ndani ya klabu hiyo kuwa rahisi.
Mazingisa ambaye ametangazwa rasmi leo Jumamosi kuchukua nafasi ya Clescentus Magori ambaye anakwenda kufanya majukumu mengine.
Amesema, kutokana na Lugha ya Kiswahili ambayo inazungumza na watu wengi wa nchi za Afrika Mashariki kuwa muhimu hivyo ni lazima ajifunze.
"Kujua Kiswahili hii itanisaidia katika majukumu yangu na kipindi chote cha maisha yangu hapa Tanzania kwa sababu sasa ndio kwenye makazi yangu,"alisema Mazingisa.
Alisema, lugha hiyo ilimvutia pia baada ya kutumika kwenye mkutano mkuu wa SADC ambao ulifanyika nchini Tanzania mwezi uliopita.
Hata hivyo, Mazingisa alipoanza mkutano wake, alianza kuzungumza kwa Kiswahili, lakini kimwonekano ni kama maneno aliyokuwa anayazungumza alikuwa anayasoma katika karatasi aliyokuwa ameiandaa. Maneno ambayo pia alikuwa akiyangumza yalikuwa yanamshinda kutamka kwa ufasaha.