Kisu chamfanya mwamuzi kuwa mbabe zaidi uwanjani

Muktasari:

Mashabiki walipigana na baadhi wakaupasua mpira uliokuwa umetumika kuchezea fainali hiyo lakini baadaye vurugu hizo zilimalizwa na mabaunsa walioingia uwanjani.

MWAMUZI wa mchezo baina ya Nonga United na Nsingwa FC, Emmanuel Paul alitoa mpya baada ya kuingia uwanjani na kisu kwa ajili ya kujilinda kutokana na eneo lililochezewa mechi hiyo ya fainali ya Kombe la Mbuzi kutokuwa na usalama.

Katika fainali hiyo iliyochezwa Uwanja wa Kigunia uliopo Mpiji jijini Dar es Salaam, mashabiki walifika kwa wingi baadhi wakiwa na shamrashamra ya ngoma huku wengine wakiwa wanavuta bangi pembeni mwa uwanja.

Wakati mechi ikiendelea mashabiki wa Nonga United walienda kumwaga chumvi langoni mwa Nsingwa FC, jambo lililomkera mwamuzi aliyeamua kuchomoa kisu na kuanza kuwakimbiza na kupelekea mechi isimame kwa muda.

Mashabiki walipoona mwamuzi anawakimbiza na kisu waliondoka eneo ambalo walikuwa wanamwaga chumvi na kurejea sehemu walikokuwa wanashangilia kwa ngoma, kuendelea na shamrashamra zao kama vile hakuna kilichotokea.

Mwamuzi aliingia uwanjani kuendelea na jukumu lake na dakika ya 60 Nonga United, ilipata bao kupitia kwa Rodrick Peter, hata hivyo bao hilo lilisababisha fainali hiyo kuvunjika baada ya wapinzani kutokubaliana nalo na kuamua kuingia uwanjani kufanya vurugu.

Mwamuzi alipoona vurugu zimezidi akaondoka, huku baadhi ya wachezaji wakitafuta namna ya kujinusuru na vurugu zilizokuwa zinaendelea. Mashabiki walipigana na baadhi wakaupasua mpira uliokuwa umetumika kuchezea fainali hiyo lakini baadaye vurugu hizo zilimalizwa na mabaunsa walioingia uwanjani.