Kisa ushangiliaji Ronaldo hatarini kufungiwa, kuikosa Ajax

Muktasari:

  • UEFA wamemfungulia kesi Ronaldo ya kufanya kitendo kisicho cha kimaadili, ambacho huenda kikasababisha kufungiwa kwa nyota huyo wa zamani wa Real Madrid.

Turin, Italia. Mshambuliaji Cristiano Ronaldo yuko hatarini kuikosa mechi ya Juventus ya robo-fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Ajax baada ya UEFA kumfungulia kesi kufuatia kushangilia ‘kihuni’.

Nyota huyo wa Ureno aliiga ushangiliaji wa Diego Simeone alioufanya katika mechi ya kwanza ya Juve ya hatua ya 16-Bora dhidi ya Atletico Madrid baada ya kufunga ‘hat-trick’ iliyowang’oa Wahispania hao katika mechi ya marudiano wiki iliyopita.

UEFA wamemfungulia kesi Ronaldo ya kufanya kitendo kisicho cha kimaadili, ambacho huenda kikasababisha kufungiwa kwa nyota huyo wa zamani wa Real Madrid.

Katika taarifa yake, UEFA imesema: “Kufuatia uchunguzi wa kinidhamu unaofanywa na Kamati ya Nidhamu na Maadili ya UEFA, kwa mujibu wa ibara ya 55 ya Kanuni za Nidhamu za UEFA (DR), kesi ya kimaadili imefunguliwa kufuatia mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16-Bora baina ya Klabu ya Soka ya Juventus na Klabu ya Atletico de Madrid, iliyochezwa Machi 12 nchini Italia.

“Kitendo kisicho cha kimaadili cha mchezaji Cristiano Ronaldo – Ibara ya 11 (2) (b) na Ibaya ya 11 (2) (d) cha Kanuni za Nidhamu za UEFA.'

UEFA imethibitisha pia kuwa watashughulikia kesi hiyo ya Ronaldo katika kikao kijacho cha Kamati ya Udhibiti, Maadili na Nidhamu Alhamisi.

Ronaldo alipigwa picha akifanya tukio hilo tata, baada ya kukamilisha ushindi wa 3-0 dhidi ya Atletico na kutinga hatua ya robo-fainali ya michuano hiyo.

Straika huyo, 34, alinakili ushangiliaji wa kocha Simeone, ambaye alifanya kitendo kama hicho baada ya timu yake kufunga goli la kuongoza katika mechi yao ya kwanza.

Simeone alitozwa faini ya Pauni 17,000 kwa tukio hilo lakini alinusurika kufungiwa kuiongoza Atletico katika mechi ya marudiano.

Kama Ronaldo atafungiwa na UEFA, huenda akakosa mechi moja ya kwanza ya Juventus ya robo-fainali mjini Amsterdam Aprili 10. Mechi ya marudiano itapigwa mjini Turin Aprili 16.