Kisa tabia: PSG yamuweka sokoni Neymar

Muktasari:

Neymar alijiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu Ufaransa kwa Pauni 198 akiwa ndiye mchezaji ghali duniani.

Paris, Ufaransa. Paris Saint Germain imekubali kumtoa mshambuliaji wake nyota Neymar katika dirisha hili la usajili.

Taarifa hiyo ni habari njema kwa miamba ya Hispania, Real Madrid na Barcelona zinazohisishwa kumtaka nyota huyo wa kimataifa wa Brazil.

PSG imesema itakuwa tayari kumpiga bei Neymar endapo itajiridhisha na thamani yake ya fedha.

Neymar alijiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu Ufaransa kwa Pauni 198 akiwa ndiye mchezaji ghali duniani.

Huenda klabu hiyo imefungua milango kwa nyota huyo kwa kuchoshwa na mwenendo mbaya wa tabia yake ndani na nje ya uwanja.

Hivi karibuni rais wa klabu hiyo Nasser Al'Khelaifi alisema anataka kila mchezaji kutunza nidhamu ndani ya klabu.

“Wachezaji wanapaswa kutambua majukumu yao. Lakini imekuwa tofauti kabisa kama mchezaji hatakubali kufuata utaratibu milango iko wazi,” alisema kigogo huyo.

Neymar amekuwa akihaha kurejesha kiwango chake kama alichokuwa nacho Barcelona tangu alipojiunga na klabu hiyo mwaka 2017 kwa Pauni198 milioni.