Kisa kukosa penalti ya Panenka mchezaji avunjiwa mkataba

Muktasari:

Bodi ya wakurungezi imekubaliana kumfukuza mchezaji wao kwa sababu ya kukosa penalti yake aliyopiga kwa mtindo wa Panenka na kukosa.

Caracas, Venezuela.Upigaji wa penalti ya Panenka umekuwa maarufu duniani na wachezaji kadhaa wakubwa wamekuwa wakipiga na kujijegea heshima kubwa kwa ujasiri wao.

Beki Sergio Ramos alipiga katika mchezo wa nusu fainali kati ya Hispania na Ureno katika Euro 2012 pia kiungo wa Italia, Andrea Pirlo alipiga dhidi ya England katika mashindano hayo.

Wakati nyota hao wakifanikiwa, lakini madhara yake ni kubwa pale mchezaji anapokosa.

Mchezaji wa Independiente de Campo Grande, Brendix Parra alikwenda kupiga penalti dhidi ya La Equidad katika mashindano ya Copa Sudamerica, lakini wakati akipiga panenka yake alikosea na mpira kumgonga kifuani kipa Diego Novoa.

Siyo tu klabu yake imeondolewa katika mashindano, ila Parra amevunjiwa mkataba wake na klabu yake kwa kukosa panenka.

“Bodi ya wakurungezi imeamua kuvunja mkataba na Brendix Parra kwa kitendo chake cha kupiga penalti kwa mtindo wa panenka,' rais wa klabu huyo Eriberto Gamarra aliimbia ABC Cardinal.

“Kama tungefanikiwa kufuzu kwa raundi ijayo kila mchezaji angepata fedha nyingi.'

Parra alionekana kuchukua uamuzi huo bila ya kinyongo kwa kusema: 'Ni hali ngumu kweli, lakini maisha lazima yaendelee.'