Kisa Taifa Stars: Kenya yamtimua kocha wake Mfaransa

Muktasari:

Kocha huyo ameiongoza Kenya kufuzu kwa mara ya kwanza kwa fainali za Mataifa ya Afrika baada ya kusubiri kwa miaka 15.

Nairobi, Kenya. Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) limesitisha mkataba wake na kocha Mfaransa Sebastien Migne.

Migne na FKK wamevunja ndoa yao ikiwa ni chini ya siku 14 tangu Kenya ilipotolewa na Tanzania katika kusaka kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan 2020).

“Shirikisho la Soka Kenya na kocha wa Harambee Stars, Sébastien Migné tumekubalia kusitisha mkataba baina yetu,” ilisomeka taarifa ya FKF.

Hata hivyo, FKF imeimshukuru Migne kwa kuiongoza Kenya kufuzu kwa mara ya kwanza kwa Afcon baada ya miaka 15.

“Shirikisho linamshukuru kocha Migné kwa kazi yake kubwa aliyofanya kwa kipindi chote alichokuwa hapa na kuiongoza timu kufuzu kwa Afcon 2019.

“Tunamtakia mafanikio mema katika kazi yake, lakini na sisi tunatakiwa kuanza kuangalia namna ya kupata mrithi wake wa kutufikisha katika fainali zijazo za Afcon 2021.

Migne ameingia katika orodha ya makocha ambao wametimuliwa kazi baada ya kushindwa kufanya vizuri katika fainali za Mataifa ya Afrika 2019.