Kisa Simba SC... Bilionea Yanga amzuia Lamine

Muktasari:

Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo, Lamine ameonekana kulegeza msimamo wa kuondoka moja kwa moja, lakini ametoa masharti manne akitaka yatekelezwe kabla ya kurejea kwake.

SAKATA la beki wa Yanga, Lamine Moro limechukua sura mpya, baada ya raia huyo wa Ghana kutoa masharti mazito kwa uongozi wa klabu yake, lakini bilionea mmoja ameingilia kati huku akimleta nchini meneja wa mchezaji huyo.

Pia, tambua kuwa Yanga tayari wamemaliza kesi ya malipo ya mishahara ya wachezaji wake baada ya zoezi hilo kukamilika jana Ijumaa na sasa shughuli imebaki kwa Lamine wakati huu ikiajiandaa na mechi zake tatu za Ligi Kuu Bara kabla ya kuvaana na watani wao wajadi, Simba mchezo ambao unatarajiwa kuwa mgumu.

Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo, Lamine ameonekana kulegeza msimamo wa kuondoka moja kwa moja, lakini ametoa masharti manne akitaka yatekelezwe kabla ya kurejea kwake.

Sharti la kwanza, ameitaka Yanga kumlipa mishahara yake ya miezi mitatu kuanzia Oktoba mpaka Desemba.

Hata hivyo, wakati Lamine akitoa sharti hilo tayari Yanga imelipa kishahara ya miezi miwili ya Oktoba na Novemba iliyoleta vurugu zote, huku wakisubiri Desemba kukamilika.

Lamine katika barua yake ameitaka Yanga kumwongezea mshahara ingawa ametoa nafasi ya majadiliano na mabosi wa klabu hiyo.

Sharti lingine ambalo huenda likawa gumu kwa Yanga ni kutaka kulipwa mishahara yake ya miezi sita zaidi ili kuondoa usumbufu wa kucheleweshewa malipo yake.

Mwisho Lamine ameitaka Yanga kuweka ahadi ya maandishi kwamba, iwapo mshahara wake utachelewa kwa mwezi mmoja na nusu basi itoshe kuvunja mkataba baina ya pande hizo.

GSM waingilia kati

Kutokana na sakata hilo na maandalizi ya mechi na Simba, matajiri wa GSM ambao ni miongoni mwa wadhamini wa Yanga, wameingilia kati na kutaka kutafuta suluhu ya haraka ili kutuliza hali ya hewa.

Mwanaspoti limeelezwa kuwa, hatua ya kwanza iliyofanywa na GSM ni kumleta nchini meneja wa beki huyo kwa majadiliano zaidi.

Mwanaspoti limezungumza na ofisa wa GSM, Hersi Said ambaye amekiri mchakato wa kumleta nchini mejena huyo umeanza kwa kumtumia tiketi ya ndege.

“Meneja wake atakuja na tumeshatuma tiketi ili tuweze kuzungumza na kupata ufumbuzi wa uhakika, Yanga wametuambia Lamine ni mmoja mzuri na anahitajika kikosini,” alisema Hersi.