Kisa Simba, Maugo kachinja mbuzi, wengine walonga

Muktasari:

  • Mbali na Maugo, bondia mwingine, Hassan Mwakinyo alisema hajawahi kujuta kuipenda Simba na katika mchezo wa juzi, alijua mabingwa hao wa Ligi Kuu watashinda tu.

UKISIKIA ushabiki basi ni huu! Eti ushindi wa juzi Jumamosi wa Simba dhidi ya AS Vita ya DR Congo umemfanya Bondia Mada Maugo kufanya sherehe na kuchinja mbuzi.

Maugo ambaye ni shabiki kindakindaki wa Simba anakwambia aliweka ahadi ya kuchinja mbuzi na kuwaalika baadhi ya mashabiki wa mpira kusherehekea endapo Simba ingeshinda.

“Hata mashabiki wa Yanga nimewaalika waje kunywa supu wapunguze machungu waliyopata tena mara mbili, kwa timu yao kufungwa, lakini pia kwa Simba kutinga robo fainali,” alisema.

Mbali na Maugo, bondia mwingine, Hassan Mwakinyo alisema hajawahi kujuta kuipenda Simba na katika mchezo wa juzi, alijua mabingwa hao wa Ligi Kuu watashinda tu.

“Nilikuwa nikiifuatilia mechi hiyo, niliposikia tumeanza kufungwa, sikujali sana, nilijua muda bado, Simba ya sasa ni habari nyingine,” alisema Mwakinyo.

Mwanariadha Gabriel Geay ambaye ni shabiki wa kulialia wa Simba anakwambia, ushindi huo ni matunda ya maandalizi bora.

“Simba kushinda hivi sasa siyo ishu kutokana na hali ya klabu ilivyo, lakini kuweka rekodi nyingine kwa kufuzu robo fainali, inastahili pongezi, ni hatua, cha msingi ijipange kwa kusonga mbele zaidi ikiwezekana hata kucheza fainali, kwani inawezekana ikiamua,” alisema.

Kocha wa Mpira wa Kikapu, Bahati Mgunda ambaye ni shabiki mkubwa wa Yanga alisema kwa hatua waliyofika Simba wanastahili pongezi, japo mashabiki wao, watachonga sana.