Kisa Simba... Yanga waitana mafichoni

WAKATI uongozi wa Yanga ukikutana na kocha mkuu, Cerdic Kaze na wasaidizi wake leo usiku kuweka mikakati kuelekea mechi ya Jumamosi, kiungo nyota wa zamani wa Simba, Mtemi Ramadhani amewataja nyota wawili wa Yanga kuwa tishio katika mechi hiyo.

Yanga itarejea Dar es Salaam leo usiku mara baada ya mechi yao na Gwambina na itakapowasili benchi la ufundi litakutana na uongozi kuweka mikakati kuelekea mechi ya watani.

Katibu Mkuu wa Yanga, Wakili Simon Patrick amesema watakuwa na kikao na benchi la ufundi leo kupanga mikakati ya mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar.

Yanga ambayo Jumamosi iliyopita iliichapa Biashara United bao 1-0 mjini Musoma na kuondoka dakika chache baada ya mechi hiyo kwenda Mwanza, kusubiri mechi na Gwambina inayochezwa leo.

Baada ya mechi hiyo Yanga itaondoka kurudi Dar es Salaam usiku wa leo kwa mujibu wa meneja, Hafidh Salehe, huku Simon akibainisha kuwa timu itaanza kambi kesho kujiandaa na Simba.

“Kikao cha kesho (leo)usiku ndicho kitaamua kama waweke kambi nje ya jiji au timu ibaki hapa hapa. Kocha ndiye atatueleza baada ya kikao, japo mpango wa kwanza ni kubaki hapa hapa Dar, ila ushauri wa kocha ndiyo utafuatwa,” alisema Wakili Simon.

Wakati Yanga wakiweka mikakati hiyo, kiungo nyota wa zamani wa Simba, Mtemi Ramadhan amewataja Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Michael Sarpong kuwa nyota watakaoisumbua Simba katika Kariakoo Derby.

Fei Toto anajitahidi sana, ana uwezo mkubwa kucheza katikati levo yake ni kama alivyo Chama ‘Clatous’ Simba, ingawa bado hajafikia kiwango alichonacho Mzambia.

“Sarpong anatumia nguvu, japo bado hajawa hatari lakini yuko fiti, ni mchezaji ambaye ukifanya kosa anakufunga, hawa ni wachezaji ambao Simba inapaswa kuwa nao makini,” alisema

Alisema kingine ambacho Yanga itajivunia Jumamosi ni ufiti wa wachezaji wake, tofauti na Simba ambayo inajivunia utaalamu wa kucheza kwa kugongeana pasi, Yanga wanakimbia na kupambana.

“Ni mechi ngumu, japo ukiingalia Simba unaweza kutabiri itashinda na Yanga watacheza kwa jihadi, ila Simba wanapaswa kutulia kweli kweli, kwani ni timu ambayo inabebwa na Chama na Miquissone ‘Luis’, ambaye pia namuona akijituma, hivyo wanapaswa kujipanga katika hilo”.

Mshambuliaji, Meddie Kagere ni miongoni mwa wachezaji wa Simba ambao imeelezwa watakosekana kwenye mechi hiyo, ingawa Mtemi amesema nahodha John Bocco ana uwezo wa kuziba pengo la Kagere.

“Bocco ana uzoefu na mechi za Simba na Yanga, ingawa hofu yangu kwa Yanga ni beki yao, Lamine Moro na Mwamnyeto ‘Bakari’ sio mabeki tishio japo wako fiti,” alisema.

Mara ya mwisho, Simba iliichapa Yanga mabao 4-1 kwenye nusu fainali ya kombe la Shirikisho, ingawa Mtemi amesisitiza si rahisi matokeo hayo kujirudia Jumamosi.