Kisa Mane, Zidane, Perez watibuana

Thursday May 23 2019

 

Madrid, Hispania. Kimewaka huko! Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane imedaiwa amewaka kufuatia Rais wa klabu hiyo, Florentino Perez kuchomoa ofa ya Mfaransa huyo ya kumvuta straika wa Liverpool, Sadio Mane.

Kwa mujibu wa taarifa iliyomnukuu, Mkuu wa mtandao wa Okdiario, Eduardo Inda alipohojiwa na kituo cha El Chiringuito, ni kwamba, Zidane na Perez ametofautiana juu ya pendekezo la kocha huyo kutaka Mane atue Bernabeu, ikielezwa tatizo mkwanja mnene.

"Zidane ametofautiana na bodi ya klabu juu ya (Thibaut) Courtois akisisitiza hana mpango naye akitaka kuendelea na kipa Keylor (Navas)," alisema Inda.

"(Kiungo wa Manchester United Paul) Pogba, yupo karibu zaidi kuliko mnavyofikiria, na ishu ya Mane ni kwamba Liverpool wametaka Euro 200 milioni na Florentino amekataa na kumtibua Zidane."

Zidane amekuwa akisisitiza kumtaka Mane, ili kukiongezea nguvu kikosi hicho ambacho msimu huu kimetoka kapa na kinachojiandaa kuachana na Gareth Bale, lakini Florentino na bodi nao wamesisitiza dau la Mane ni kubwa mno. Badala yake Rais huyo alitaka kuwapa ofa ya muda mrefu Vinicius Junior na Marcos Asensio kuliko kumchukua Mane aliyemaliza msimu katika Ligi Kuu ya England akifunga mabao 22 sawa na pacha wake pale Anfield, Mohammed Salah na Pierre Emerick Aubameyang wa Arsenal.

Advertisement