Kisa Hakimu Mgonjwa kesi ya kupinga uchaguzi Yanga yahairishwa Aprili 29

Muktasari:

  • Kesi hiyo ya kikatiba namba 1 ya mwaka 2019, iliyofunguliwa, Januari 11, 2019, na wanachama wawili wa Klabu ya Yanga, Juma Magoma na Athman Nyumba dhidi ya bodi ya wadhamini wa klabu ya Yanga na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Aprili 29 mwaka huu kusikiliza kesi ya kupinga uchaguzi wa Klabu ya Yanga, upande mmoja bila wadaiwa kuwepo baada ya kushindwa kuitikia wito wa kufika mahakamani hapo.

Hata hivyo, kesi hiyo ilipaswa kusikilizwa leo katika mahakama hiyo, lakini iliahirishwa kutokana Hakimu anayesikiliza shauri, Janeth Mtega kuwa ni mgonjwa na hivyo kushindwa kusikiliza kesi hiyo.

Kutokana na hali hiyo, kesi hiyo imeahirishwa hadi April 29, 2019 itakapoendelea.

Kesi hiyo ya kikatiba namba 1 ya mwaka 2019, iliyofunguliwa, Januari 11, 2019, na wanachama wawili wa Klabu ya Yanga, Juma Magoma na Athman Nyumba dhidi ya bodi ya wadhamini wa klabu ya Yanga na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Katika kesi hiyo, wadai, Magoma na Nyumba wanapinga kufanyika kwa uchanguzi huo kwa madai kuwa unakwenda kinyume na katiba ya Klabu ya Yanga ya mwaka 2010, ibara ya 7.

Hata hivyo tangu kesi hiyo ilipofunguliwa wadaiwa hawajawahi kufika mahakamani licha ya kupelekewa wito wa mahakama mara kadhaa na hata kutangazwa gazetini.

Kutokana na hali hiyo upande wa wadai kupitia kwa Wakili wao Daudi Mzeri, Aprili 8, mwaka huu aliiomba mahakama hiyo iamauru kesi hiyo iendelee kusikilizwa upande mmoja, akidai kuwa imekuwa vigumu kwa mdaiwa huyo kupoikea hati ya wito iliyotolewa na mahakama.

Wakili Mzeri alidai kuwa licha ya Mahakama hiyo kuamuru, Bodi ya wadhamini wa Klabu ya Yanga kutangazwa katika gazeti la Uhuru kama njia ya wito wa kufika mahakamani hapo, bado imekuwa vigumu kufika mahakamani hapo kusikiliza shauri hilo.

“Kutokana na wadaiwa wote kushindwa kufika mahakamani hapa licha ya mahakama kuamuru mdaiwa wa pili (Bodi ya wadhamini wa klabu ya Yanga) atangazwe gazetini, lakini bado wameshindwa kufika mahakamani kusikiliza shauri lao, pia hata Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) naye ameshindwa kufika mahakamani hapa” alidai wakili Mzeri na kuongeza

“Kesi hii imetajwa mara tatu kwa maana ya Februari 11, Machi 11 na April 8, bila wadaiwa kufika mahakamani kusikiliza shauri hili, hivyo kutokana na hali hii tunaiomba mahakama isikilize shauri hili upande mmoja” alidai Mzeri

Wakili Mzeri alidai kuwa mdaiwa wa pili katika shauri hilo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), alitangazwa Februari 8, 2019 kupitia gazeti la Uhuru, huku mdaiwa wa kwanza, yeye hajatangazwa gazetini kwa sababu alipokea wito wa mahakama, lakini hakufika mahakamani.

Uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Januari 13, 2019 kwa lengo la kujaza nafasi mbalimbali zilizoachwa wazi, lakini ulishindikana kutokana na kufunguliwa kwa kesi hiyo.

Katika madai yao Magoma na Nyumba wanapinga kufanyika kwa uchaguzi huo kwa madai kuwa unakwenda kinyume na katiba ya Klabu ya Yanga ya mwaka 2010 ibara ya 7.

Ibara hiyo inaelezea utaratibu wa uanachama ndani ya Klabu ya Yanga ambao, kwanza ni kutuma maombi, ambapo maombi hayo yatapelekwa kwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga, ambaye baaade yatajadiliwa na kamati tendaji.

Pia, ibara hiyo, inaelezea kuwa maombi hayo yataambatana na fomu namba YASC/U, ada ya uanachama ambayo ni Sh 12,000 pamoja ana ada ya kadi ambayo ni Sh 2000.

Pia wanadai kuwa kuna taarifa za kuwepo kwa wanachama wenye kadi feki za kieletroniki ambazo zina saini na mhuri ambazo zinasambaa kwa baadhi ya wanachama, ambazo zinaonyesha kuwa zimetolewa na benki ya CRDB pamoja na benki ya Posta.

Wanadai kuwa kadi hizo zinazodaiwa kuwa ni kadi za uanachama wa Klabu ya Yanga, zikiwa na picha za wamiliki ambazo sio mali ya klabu hiyo.

Hivyo wanapinga matumizi ya kadi hizo katika uchaguzi huo wakidai kuwa kwa namna yoyote ile haziwezi kuwa uthibitisho wa uanachama wa Yanga, kwa kuzingatia kwamba, wahusika wa hizo kadi, hawakupitia utaratibu ulioanishwa katika ibara ya 7 ya mwaka 2010 ya klabu ya Yanga.

Wanachama hao wanapinga kumpa mtu uanachama bila kadi hiyo kusainiwa na kugong’wa mhuri wa klabu, hivyo haiwezi kutumika kuainisha uanachama wenye haki ya kupiga kura katika uchaguzi wa klabu ya Yanga.

Wanadai kuwa utaratibu wa kadi za uanachama zilizotolewa na benki hizo, mpaka sasa haufahamiki wala hauna uthibitisho katika katiba ya Yanga.

Nafasi za uongozi zilizo wazi katika Klabu ya Yanga ni pamoja na uenyekiti, ambayo aliyekuwa mwenyekiti, Yusufu Manji alijiuzuru na makamu wake Clement Sanga, pamoja na wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji.

Wajumbe hao waliojiudhuru ni Hashimu Abdallah, Salum Mkemi, Omari Saidi na Ayub Nyenzi.