Kisa Aussems, Kagere afunguka

Muktasari:

Baada ya kutamba msimu uliopita, mambo hayakuwa mazuri kwa Aussems msimu huu kwani, walijikuta wakiondoshwa mapema na UD Songo ya Msumbiji raundi ya awali kwa sheria ya bao la ugenini.

STRAIKA wa Simba, Meddie Kagere ‘MK 14’ amesema licha ya mambo yanayoendelea kumhusu Kocha Patrick Aussems, lakini ni miongoni mwa makocha bora waliomfundisha soka la ushindani.

Huu ni msimu wa pili kwa Kagere kuwa chini ya Aussems, ambaye kwa sasa amesimamishwa kazi kufuatia kuondoka nchini bila kuwaaga viongozi wake. Kagere, ambaye msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara na mchezaji bora wa mwaka wa Simba, alisema ubora wa Aussems unatokana na mbinu alizonazo zilizowasaidia kufanya vizuri msimu uliopita ikiwemo michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Sikuwepo Tanzania wakati ishu yake inatokea, nilikuwa na majukumu ya timu ya Taifa, nilisikia juujuu, kwangu ni kocha bora alitufanya tujiamini na kufanya vizuri msimu uliopita kwenye Ligi ya Mabingwa,” alisema.

Simba ikiwa chini ya Aussems ilitinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ambapo ilitolewa kwa kipigo cha jumla cha mabao 4-1 na TP Mazembe ya DRC.

Nyota alisema: “Tulikuwa na nafasi hata msimu huu pia kufanya vizuri, lakini hatukuwa na hesabu nzuri katika mchezo wa marudiano hasa baada ya kupata suluhu tukiwa ugenini. Tuliteleza na haina maana kuwa hatukuwa na ubora wa kusonga mbele.”

Baada ya kutamba msimu uliopita, mambo hayakuwa mazuri kwa Aussems msimu huu kwani, walijikuta wakiondoshwa mapema na UD Songo ya Msumbiji raundi ya awali kwa sheria ya bao la ugenini. Kagere mwenye mabao manane katika ligi, alisema hata kuteuliwa kuwania tuzo za uchezaji bora wa Afrika kwa klabu za ndani kumechangiwa na Aussems ambaye alikuwa akimuamini kila mchezo na kumpa nafasi.