Kisa 1.2 Bil... Simba yamponza Kessy Zambia

Saturday December 8 2018

 

By CHARLES ABEL

NI wazi beki Mtanzania anayecheza Nkana Red Devils ya Zambia, Hassan Kessy anatafuta namna ya kuwamaliza Simba wakati watakapokutana kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Bila shaka ndoto ya Kessy ni kufikia rekodi ya Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ambao, wamecheza hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika zaidi ya mara mbili.
Kabla ya hapo, Kessy alicheza hatua hiyo akiwa na Yanga mwaka 2016 na 2018 kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya kutimkia Zambia.
Kama ilivyo kwa Kessy, Simba nao wamepania kuing'oa Nkana ili iweze kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo kitemi mwaka 2003.
Lakini, Simba wana tamaa ya kuvuna Dola 550,000 (zaidi ya Sh 1.26 bilioni) ambacho kila timu iliyoingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hupewa hata kama imeshika mkia.
Lakini, wakati suala la kufuzu hatua ya makundi na donge nono la fedha yakitarajiwa kuwaingiza vitani Kessy na Simba, hofu ya kukutana na miongoni mwa timu 20 tishio kwenye Kombe la Shirikisho huenda ukafanya mechi baina ya Simba na Nkana ikawa na ushindani mkubwa.
Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) timu inayotolewa kwenye Ligi ya Mabingwa inapata fursa ya kuingia hatua ya mwisho ya mtoano ya Kombe la Shirikisho kwa ajili ya kupata timu zitakazofuzu makundi.
Wakati wengi wakiamini Kombe la Shirikisho huwa na timu nyepesi safari hii kuna vigogo wengi ambao mmoja atakutana na Simba na Nkana.
Vigogo hivyo ni Étoile du Sahel na CS Sfaxien za Tunisia, Hassania Agadir, Raja Casablanca na RS Berkane (Morocco), USM Bel Abbès na NA Hussein Dey (Algeria), Zamalek na Al-Masry (Misri), Al-Ahli Tripoli na Al-Ittihad (Libya), Green Buffaloes (Zambia) na Kaizer Chiefs (Afrika Kusini).
Timu nyingine ni Asante Kotoko (Ghana), Enugu Rangers (Nigeria), KCCA (Uganda), DC Motema Pembe (DRC), Al-Hilal Al-Ubayyid (Sudan), Génération Foot (Senegal) na Mtibwa Sugar ya Tanzania.
Timu hizo nyingi zinasifika kwa uwekezaji mkubwa wa fedha na kuwa na wachezaji wa daraja la juu, mafanikio kwenye mashindano ya klabu Afrika yaliyofanyika miaka ya hivi karibuni, lakini pia ubora wa ligi za nchi zao.
Mchambuzi wa soka na nahodha aliyeiongoza Yanga kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998, Ally Mayay alisema Simba inapaswa kuitupa nje Nkana na sio kufikiria Kombe la Shirikisho.
"Ligi ya Mabingwa ndio lengo kuu na ndoto ya kila timu hivyo kuna haja kwa Simba kuhakikisha wanafanya kila liwezekanalo ili waweze kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu huu.
Mechi zao mbili dhidi ya Nkana zitakuwa ngumu, lakini Simba msimu huu wana kikosi kipana chenye wachezaji bora ambao wanaweza kuwapatia matokeo dhidi ya timu yoyote ile iwapo watajipanga vizuri hivyo sioni cha kuhofia kwao," alisema Mayay.

Advertisement