Kipigo cha Yanga chamvuruga straika wa kigeni Mbeya City

Tuesday September 15 2020

 

By MASOUD MASASI

MWANZA. BAADA ya kuchezea kichapo kwenye michezo miwili, Straika Mnigeria wa Mbeya City, Abasirim Chidiebere amekiri mambo ni mazito kwao kwenye Ligi Kuu, hivyo wanachotakiwa sasa ni kupambana vilivyo ili kuanza kupata ushindi ambao utawarejeshea nguvu kubwa.

Mbeya City walianza kwa kichapo cha 4-0 kutoka kwa KMC kisha Jumapili ya wiki iliyopita walichezea kichapo cha 1-0 kutoka kwa Yanga.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chidiebere alisema hali imeshakuwa mbaya kwao kwani kupoteza mechi mbili ni jambo baya, hivyo sasa wanatakiwa kukomaa vilivyo ili mechi zijazo waweze kupata ushindi.

Alisema vichapo hivyo vimewaumiza sana wachezaji, hivyo ni wakati sasa wa kupambana ili waweze kupata matokeo mazuri ndani ya uwanja.

“Tumepoteza mechi mbili za ligi, ni kitu kibaya kwetu, hivyo tunatakiwa tukomae sana ili mechi zijazo tuweze kupata ushindi wa kwanza ambao utatupa nguvu upya za kupambana kwenye mashindano haya,” alisema Chidiebere.

“Kocha ameona upungufu wetu, hivyo ataufanyia kazi kwani kila mtu hajafurahi kutokana na matokeo haya tuliyopata kwenye hizi mechi mbili, kikubwa ni kujipanga upya ili tuweze kufanya vizuri.”

Advertisement

Alisema ligi ni ngumu na wanachotakiwa kufanya ni kuongeza juhudi kwenye mechi watakazocheza ili kuweza kufanya vizuri, la sivyo mambo yatazidi kuwa mabaya kwao msimu huu.

Advertisement