Kipigo Kagera Sugar chamnyima raha Aussems

Muktasari:

 

  • Kocha raia wa Ubelgiji alisema Kagera imewaachia maumivu benchi la ufundi na wachezaji aliodai kila mmoja amesikitishwa na matokeo hayo.

Dar es Salaam. Jinamizi la kipigo cha mabao 2-1 ilichopata Simba dhidi ya Kagera Sugar, bado kinamuandama Kocha Patrick Aussems.

Simba juzi ilikwaa kisiki baada ya kupoteza mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Akizungumza kwa simu jana, Aussems alidai kipigo hicho kimetibua mipango yake kwa kuwa mkakati wake ulikuwa ni kuendeleza wimbi la ushindi katika mechi zake zilizobaki.

“Sikutarajia kupata matokeo haya, timu ilicheza chini ya kiwango hasa dakika 45 za kipindi cha kwanza. Hata kipindi cha pili tulicheza tu ili tukamilishe mchezo,” alisema Aussems.

Kocha raia wa Ubelgiji alisema Kagera imewaachia maumivu benchi la ufundi na wachezaji aliodai kila mmoja amesikitishwa na matokeo hayo.

Alisema Kagera ilistahili kupata pointi tatu kwa namna ilivyocheza kulinganisha na wachezaji wake aliodai walicheza kichovu.

Pia Aussems alizungumzia namna atavyokuwa akicheza mechi za viporo Kanda ya Ziwa dhidi ya Alliance ya Mwanza, KMC na Biashara United ya mkoani Mara.

Kocha huyo alisema atakuwa akifanya mabadiliko ya kikosi kulingana na aina ya mchezo ingawa mkakati wake ni kushinda mechi zote za Kanda ya Ziwa.

“Kila baada ya siku mbili tunatakiwa kucheza mechi tukiwa tunasafiri, kwa maana hiyo tutakuwa tunacheza mechi ambazo zitakuwa ngumu, lakini kulingana na wachezaji wangu nitafanya mabadiliko ya kikosi kila mechi,” alisema Aussems.

Kocha huyo alisema kitendo cha wachezaji kukosa muda wa kupumzika kinaweza kuathiri malengo yake ya kuvuna pointi katika kila mchezo.

Kesho Simba itakuwa Uwanja CCM Kirumba, Mwanza kuvaana na Alliance ambao katika mechi ya kwanza iliichapa mabao 5-0 jijini, Dar es Salaam.

Tangu kuanza msimu huu Simba imepoteza mechi ya pili katika Ligi Kuu baada ya kufungwa mzunguko wa kwanza na Mbao FC bao 1-0.

Matokeo hayo yameongoza ushindani kati ya Simba, Yanga na Azam ambazo kila moja ina nafasi ya kutwaa ubingwa.

Kabla ya Simba kufungwa na Kagera, Yanga ilichapwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Pia Azam ilichapwa bao 1-0 na Ndanda mkoani Mtwara.

Yanga inaongoza katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 74, Azam (66) na Simba ambao ni mabingwa watetezi 60. Wakati Yanga na Azam zikiwa zimecheza mechi 32 Simba ambao ni mabingwa watetezi imeteremka uwanjani mara 24.