Kipigo Gor chatesa Kahata, Oliech afunguka mazito

Saturday January 26 2019

 

By THOMAS MATIKO

KIUNGO wa Gor Mahia,Francis Kahata amesema bahati tu iliwabeba Mbao FC katika mchezo wao wa robo fainali ya mashindano ya Sport Pesa huku straika Denis Oliech akiwa haamini kilichotokea.

Gor Mahia ambao walikuwa mwabingwa watetezi wa mashindano hayo walitolewa hatua hiyo baada ya kufungwa na Mbao FC kwa penalti 4-3 baada ya dakika 90 kutoka sare ya bapo 1-1.

Kahata ambaye aliingia kipindi cha pili katika mchezo huo alisema waliupiga mpira mwingi lakini bahati haikuwa yao.

“Tulicheza vizuri kuanzia kipindi cha kwanza hata cha pili. Kutotumia nafasi nyingi tulizopata kulitugharimu na mwisho kwenda kwenye penalti na kutolewa.

“Niseme wapinzani wetu(Mbao) walikuwa na bahati tu katika mchezo huo kwani kama tungeongeza nguvu kidogo na kuwa makini tusingefika kwenye matuta,” alisema Kahata.

“Yaani bado siamini tumechujwa. Nilikuwa na motisha sana na shindani hili na kusema kweli nilifikiri tungesonga hadi fainali na kushinda tena. Mbao walibahatika tu, kwa sababu kama wachezaji tulijituma sana ila haikuwa siku yetu,” alisema Oliech baada ya kurejea nchini.

Katika mchezo huo Gor Mahia ndio ilikuwa ya kwanza kufunga bao dakika ya 52 lililofungwa kwa Penalti na Dennis Oliech kabla ya Mbao kusawazisha dakika ya 76 kupitia kwa Raphael Siame.

Katika mikwaju ya penalti,Gor Mahia walifunga kupitia kwa Francis Kahata,Jacques Tuyisenge na Boniface Omond wakati Harun Shakavah na Shafiq Batambuze walikosa.

Mbao ilifunga penalti zao kupitia kwa Said Khamis,Raphael Siame,Hamimu Abdukarim na David Mwasa wakati Hashimu Ibrahim alikosa.

Oliech alisema anageuza nguvu zake kuisaidia Gor kutetea ubingwa wa Ligi Kuu.

Advertisement