Kipchoge hoi, Kitata Bingwa

BINGWA wa mtetezi wa London Marathon, Eliud Kipchoge ameshindwa kutamba katika mbio hizo zilizofanyika jana na kushuhudia, Shura Kitata raia wa Ehiopia akiibuka bingwa.

Kabla ya mbio hizo Kipchoge alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kutetea ubingwa na kupata ushindani kutoka kwa Kenenisa Bekele ambaye alijitoa mapema.

Kitata alitumia saa 2:05:41 wakati msimu uliopita alimaliza nafasi ya nne akitumia saa 2:05:01, hivyo licha ya msimu huu kuibuka kinara alishindwa kuboresha muda wake zaidi.

Haikua siku njema kwa Kipchoge aliyemaliza nafasi ya nane kwa saa 2:6:49 wakati msimu uliopita aliibuka kinara akitumia saa 2:2:37.

Wanariadha kutoka Ethiopia walitawala mbio hiyo kwani pamoja na Kitata kuwa bingwa lakini walitawala hadi nafasi ya sita. Nafasi ya pili ilikamatwa na Vincent Kipchupa aliyetumia saa 2:5:42 na nafasi ya tatu ikimalizwa na Sisay Lemma aliyemaliza nafasi hiyo baada ya kutumia saa 2:5:45.

Kwa upande wa kina dada bingwa mtetezi, Brigid Kosgei raia wa Kenya aliendeleza ubabe wake ubingwa mwingine na kunyakua kitita cha Dola 30,000 (Sh.69 milioni) kwa kutumia saa 2:18:58 na .

Nafasi ya pili ikienda kwa Sara Hall aliyetumia muda wa saa 02:22:01 na nafasi ya tatu ilishikwa na Ruth Chepngetich akitumia saa 02:22:05.

Tanzania imeendelea kuwa watazama kwenye mbio hizo kwani ni msimu wa tatu haijapata mwakilishi na mara ya mwisho Tanzania kushiriki ilikuwa mwaka 2017, pale Alphonce Simbu alipomaliza nafasi ya tano akitumia saa 2:9:10.

Mwaka juzi Simbu alipata mwaliko lakini kutokana na kubanwa na majukumu yake hakuweza kushiriki na hadi sasa hakuna mtanzania aliyepata nafasi ya kwenda huko.

Mbio hizo zimefanyika mara 40 lakini Tanzania imeendelea kuwa watazamaji wa wanariadha kutoka Kenya na Ethiopia.

Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) inapaswa kutazama namna ya kurejesha morali ya mchezo huo kwani inaonekana kila mmoja hana muda wa kuupigania mchezo huo na kuwafanya wanariadha wetu kuwa washindani.