JICHO LA MWEWE: Kipa wetu Kabwili anapopata ajali ya Bodaboda

MAJUZI nilitabasamu katika habari mbaya. Mdogo wangu, Ramadhan Kabwili alipata ajali ya bodaboda huko uswahili anakoishi. Kwanini mwanadamu unatabasamu katika ajali mbaya? Kitu cha kushangaza. Hata hivyo wakati mwingine tunalazimishwa kutabasamu.

Hizi Bodaboda zina madhara sana. Ni usafiri kama usafiri mwingine wowote lakini zina madhara sana. Ukienda katika wodi za watu wenye matatizo ya mifupa nchini kote utakutana na watu wengi zaidi waliopata ajali za bodaboda kuliko ajali za kawaida.

Takwimu hazidanganyi. Tunaweza kujidanganya kuwa ajali ni ajali lakini ukweli unabakia pale pale kwamba namba hazidanganyi. Bodaboda unabakia kuwa usafiri wa hatari zaidi kuliko usafiri mwingine wowote kwa sasa nchini.

Ipo siku ambayo nilikwenda kutembelea Wodi ya Moi pale Muhimbili. Miguu mingi imening’inia kwa sababu ya ajali za bodaboda. Wakati ule tajiri wa Simba, Mohamed Dewji alipowapa wachezaji wa Simba zawadi ya bodaboda nilitafakari kidogo. Aliwapa ili waende kuwahi mazoezini au aliwapa ili wafanyie biashara?

Turudi kwa Kabwili. Wachezaji wetu wajitambue kidogo. Namba za ajali za bodaboda haziongopi. Ni usafiri wa hatari. Kabwili anatambua thamani yake? Ni mchezaji wa Yanga. Ukubwa wa timu unapaswa kumfanya aishi maisha tofauti kidogo.

Kuna mambo mengi. Kwanza kabisa anayaweka maisha yake ya soka hatarini. Akiumia hataweza kukifanya kitu ambacho anaweza kukifanya vizuri zaidi katika maisha yake ya kileo. Kucheza soka. Amesoma? Sina uhakika kama ana elimu ambayo inaweza kumsababishia apate maisha mazuri nje ya soka.

Katika hili amenishangaza Kabwili na wananishangaza pia baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu waliojikita kucheza michuano ya mchangani. Hawajui kama wanahatarisha maisha yao katika kitu ambacho hakiwezi kuhesabiwa katika hesabu za bima.

Kama Kabwili ana bima ya soka nadhani hawezi kulipwa katika madhara anayoyapata na ajali ya bodaboda. Na kama kuna mchezaji wa Ligi Kuu amewekewa bima sidhani kama anaweza kulipwa katika ajali ya mechi ya mchangani.

Tatizo kubwa la wachezaji wetu ni kwamba wanadharau kazi zao. kazi hizi hizi ambazo wanaamini haziwalipi vizuri basi kuna watu wanazitamani. Wanapaswa kuziheshimu na kujaribu kuishi kwa kujilinda zaidi.

Lakini wachezaji wetu pia wajaribu kutazama kitu kinachoitwa Brand. Siku hizi hili neno limekuwa maarufu. Kiswahili sahihi sijui ni kipi lakini nadhani wanamaanisha katika kumpandisha chati mtu maarufu awe na hadhi zaidi.

Kwa mfano, hauwezi kumkuta Diamond Platinum anapanda bodaboda ana-katisha mtaani. Watu wata-sha-ngaa sana. Hadhi yake ni kubwa. Kwa sasa hauwezi kumkuta Mbwana Samatta amepanda Bodaboda. Watu watashangaa sana. Inahitajika dharura iliyopitiliza kwa Diamond kupanda bodaboda. Labda kama wanakaribia kuachwa na ndege.

Pale uwanja wa Taifa nimewahi kumuona rafiki yangu, Shiza Kichuya akiondoka na bodaboda baada ya mechi fulani ya Simba kumalizika. Ni kweli kwamba alikuwa ameomba ruhusa akaendelee na mambo yake na hivyo kuliacha basi la timu, lakini ndio upande bodaboda?

Shabiki anajisikiaje wakati anapomuona mchezaji mwenye hadhi, wa Simba, akipanda bodaboda dakika chache baada ya kumalizika kwa mechi? Shabiki ametoka kulipa kiingilio kikubwa kumtazama staa wake akicheza, lakini ghafla shabiki anaingia katika gari lake zuri na mchezaji anayempenda anampita akiwa katika bodaboda. Maisha gani haya?

Kina Kabwili wajaribu kujitengenezea hizi hadhi. Hata kama hawana pesa sana lakini mchezaji wa Yanga au kifupi mchezaji wa Ligi Kuu ni mtu mkubwa. Anapaswa kuheshimika. Kama ni kuendesha pikipiki basi iwe binafsi na yenye thamani kubwa tofauti na hizi bodaboda tulizozizoea.

Zamani kulikuwa na wachezaji ambao walikuwa na hadhi kubwa na ambao walikuwa wakiishi maisha ya tofauti kidogo. Walionekana kuwa mabishoo lakini ukweli ni kwamba walitambua hadhi ya klabu walizokuwa wanachezea.

Mfano ni Hussein Marsha. Hata kama zamani kungekuwa na bodaboda bado Hussein ninayemfahamu asingeweza kupanda bodaboda. Ni yule yule Hussein ambaye alikuwa hachezi mechi za mitaani. Katika dunia ya leo ambao wachezaji wana kipato kikubwa zaidi unadhani Hussein angecheza? Hapana.

Klabu zetu zina watu wa kuongea na hawa vijana? Wanaweza kuwa wanamshauri apande bodaboda? Siamini kama watu hao wapo.