Kipa wa Harambee Stars, akaribia kutua St. George

Mlinda mlango wa Harambee Stars, Patrick Matasi.

Muktasari:

  • Kama Patrick Matasi atajiunga na klabua ya St. Georges, atakuwa ni Staa wa 13, katika kikosi cha Stars cha sasa kinachoongozwa na mfaransa Sebastien Migne.

Nairobi, Kenya. Mlinda mlango wa Harambee Stars, Patrick Matasi yuko mbioni kujiunga na klabu ya St. George ya Ethiopia, Mwanaspoti Digital Imefahamu.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka nchini Ethiopia, zinasema mazungumzo kati ya Matasi, anayekipiga katika klabu ya Tusker FC ya humu nchini na ambaye alikuwa langoni, siku ya Jumapili Kenya ilipoitandika Ethiopia 3-0 kwenye mechi ya kusaka nafasi ya kufuzu kombe la mataifa ya Africa, yameshaanza.
Matasi aliondoka nchini mapema leo kuelekea Mjini Addis Ababa, Ethiopia na inaaminika kuwa Kipa huyo, ambaye mpaka sasa hajafungwa katika mechi tisa alizo kaa langoni, amepokea ofa babkubwa kutoka kwa St. George.
Mapema juma hili, kulikuwa na taarifa kuwa, Klabu hiyo ambayo ni moja ya klabu kubwa katika soka la bars la Africa, liliamua kusitisha mpango wa kumsajili Matasi na kuhamishia nguvu zao kwa Kipa wa Mali, Sory Ibrahim Traore, kutokana na mazungumzo kati yao na Tusker FC, kuonekana kutokuwa na muafaka.
Endapo dili hilo litafanikiwa, Matasi ambaye amewahi kuitumikia Posta Rangers nabla ya kujiunga na klabu yake ya sasa mwanzoni mwa mwezi Juni, atakuwa mrithi wa nafasi iliyoachwa na Mganda, Robert Odongkara, baada ya jaribio la kumpata Mghana Muntari Tagoe, kugonga ukuta.