Kipa Yanga mtegoni

Muktasari:

Yanga inashika nafasi ya pili ya Kundi B wamebakiza mechi mbili ambapo leo Jumatatu usiku wanacheza na Malindi ambapo mechi ya mwisho watakutana na Jamhuri.

KIPA Ibrahim Hamid ndiye anayesimama langoni mwa Yanga kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani hapa na juzi Jumamosi usiku alifungwa mabao 3-0 na Azam uwanja wa Amaan.
Mabao hayo ya Azam yalifungwa na Obrey Chirwa, nyota wa zamani wa Yanga pamoja na Enock Atta walioonekana kuwa mwiba kwenye ngome ya Yanga.
Hamid ni usajili mpya wa makipa kwenye kikosi cha Yanga akitokea timu ya taifa ya Ufukweni na anapaswa kujipanga kwa mechi zilizosalia ili asiiendelee kutunguliwa.
Yanga imekiri, wamekubali matokeo, lakini wameelezea mabao yote matatu kuwa yana sababu, japo malengo yao ya kuingia kwa kucheza sana pembeni yalifeli.
"Bao la kwanza tunamlaumu mwamuzi hakutenda haki, bao la pili na tatu ni uzembe wa beki na kipa. Tuliingia na malengo ya kucheza sana pembeni ili tupate matokeo mazuri baada ya kuwasoma wapinzani wetu lakini mpango huo ulifel," alisema Menaja Nadir Haroub 'Cannavaro' aliyeongeza;
"Lakini mpira ndivyo ulivyo na tunakubaliana na hayo yote tunajipanga kwa ajili ya mechi ijayo, wapinzani wetu wamefanikiwa mipango yao na wamecheza vizuri kutimiza lengo."
Yanga ambayo inashika nafasi ya pili sasa kundi B wamebakiza mechi mbili ambapo leo Jumatatu usiku wanacheza na Malindi ambapo mechi ya mwisho watakutana na Jamhuri.