Kipa Simba azua balaa Ethiopia

Muktasari:

Daniel Agyei (30), aliichezea Simba kwa msimu mmoja wa 2016/2017 akiiwezesha kumaliza ikiwa nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu huku pia akitoa mchango kwa timu hiyo kutwaa Ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam

Kipa wa zamani wa Simba, Daniel Agyei ameiponza timu ya Jimma Abar Jifar ya Ethiopia baada ya klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Ethiopia kufungiwa usajili katika madirisha matatu kutokana na kutomlipa stahiki zake.

Kamati ya usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), jana Agosti 11 iliamua kuwa klabu hiyo inatakiwa kumlipa Agyei, madai yake yote adhabu ambayo itaenda na kifungo cha kutosajili kwa madirisha matatu mfululizo.

Katika usikilizaji na usuluhishi wa shauri hilo lililofunguliwa na Agyei tangu Aprili 15 mwaka huu, kamati hiyo ya usuluhishi ya FIFA, imegundua kuwa klabu hiyo ya Jimma Abar Jiffar imekiuka makubaliano ya kimkataba baina yao na kipa huyo jambo ambalo ni kinyume na muongozo wa hadhi za wachezaji.

Kwa mujibu wa uamuzi huo uliotolewa na FIFA, Klabu hiyo ya Ethiopia imetakiwa kuhakikisha inalipa stahiki za Agyei ndani ya muda mfupi tangu adhabu hiyo ilipotangazwa na kama ikishindikana kamati hiyo itaongeza adhabu zaidi kwa klabu hiyo.

Agyei alijiunga na Jimma Abar Jifar mwaka 2017 akitokea Simba ambaqyo ilimsajili mwaka 2016 kutokea klabu ya Medeama ya Ghana.

Kipa huyo aliwahi kuiongoza timu ya Taifa ya Vijana ya Ghana kwa umri chini ya miaka 20, kutwaa ubingwa wa mashindano ya Afrika na Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo mwaka 2009 lakini pia alikuwemo katika kikosi cha timu ya Taifa ya Ghana ‘Black Stars’ kilichoshiriki Fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini mwaka 2010 ambacho kiliishia hatua ya robo fainali.

Ndani ya msimu mmoja alioichezea Simba, kipa huyo aliiwezesha kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam na pia pia kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu nyuma ya Yanga iliyotwaa ubingwa.