Kipa Azam aibukia Asante Kotoko

Muktasari:

Abalora ameichezea Azam FC kwa misimu mitatu akionyesha ubora mkubwa licha ya kulalamikiwa kufanya makosa ya mara kwa mara yaliyoigharimu klabu yake.

MILINGOTI ya Azam FC kwa sasa iko chini ya mikono salama ya David Kissu, ambaye wamemnasa kutoka Gor Mahia ya Kenya hivyo kumfungulia milango kipa wao Razack Abalora.

Mabosi wa Azam waliamua kumalizana na Abalora wakati huo akiwa nchini kwao Ghana alipokwenda kutualia baada ya ligi kusimama kutokana na janga la corona.

Baada ya kuvunja mkataba huo Azam walimnasa Kissu, ambaye tangu msimu huu umeanza ameruhusu mabao mawili dhidi ya Kagera Sugar, lakini Abalora naye amenasa dili baada ya kusaini mkataba wa kuwatumia wababe wa soka la Ghana, Asante Kotoko.

Mapema leo Jumanne Oktoba 13, 2020, mabosi wa Asante Kotoko wamemtangaza rasmi Abalora akisaini mkataba wa miaka mitatu kama mchezaji huru.

Abalora ameitumikia Azam FC kwa miaka mitatu baada ya kusajiliwa mwaka 2017 akitokea West African Football Academy (WAFA) ya Ghana.

Kwa sasa Asante Kotoko inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Ghana na kesho Jumatano itashuka dimbani kukipiga na Eleven Wonders FC.