Kipa Arsenal azimia Italia

Muktasari:

 

  • Kipa huyo alipatiwa huduma ya haraka kabla ya kuwahishwa katika hospitali ya jirani.

Milan, Italia. Kipa David Ospina wa Arsenal ambaye yuko kwa mkopo Italia, alikimbizwa hospitalini baada ya kugongwa kichwani wakati akiitumikia Napoli katika mechi ya Serie A dhidi ya Udinese usiku wa kuamkia leo.

Ospina, 30, alichanika kichwani baada ya kugongana na winga wa Udinese, Ignacio Pussetto, katika dakika ya saba tu ya kipindi cha kwanza.

Kipa huyo wa Colombia alitibiwa haraka baada ya ajali hiyo mbaya iliyomwacha na jeraha kichwani lakini aliweza kuendelea kucheza.

Baada ya kutibiwa, Ospina aliruhusu magoli mawili kabla ya kuanguka akiwa peke yake katika dakika ya 44, na kuwafanya wachezaji wenzake waliojawa hofu kuita machela.

Kipa huyo alipatiwa huduma ya haraka kabla ya kuwahishwa katika hospitali ya jirani.

Alex Meret alichukua nafasi ya Ospina kabla ya mapumziko. Napoli walishinda 4-2.