Kipa Aigle Noir aitaka Stars

Monday September 14 2020

KIPA Mtanzania, Erick Johora anayeidakia Aigle Noir ya Ligi Kuu Burundi, ameonyesha kuwa na dhamira ya kuichezea timu ya taifa la Tanzania maarufu kama Taifa Stars.

Kipa huyo ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Aigle Noir ambacho kilitandikwa mabao 2-0 dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa katika mechi ya kirafiki ya kilele cha Wiki ya Mwananchi, anaamini Mungu atamsimamia.

Johora alisema kama ambavyo haikuwa rahisi kwake kupata nafasi ya kucheza soka Burundi ndivyo ambavyo anaona itawezekana pia kuichezea Taifa Stars miaka michache ijayo.

“Kwa miaka yangu bado nina nafasi ya kuichezea Taifa Stars, ninachoshukuru Mungu ni kwamba nimetoka nyumbani mapema hata kama hii sio ligi kubwa kihivyo ninayocheza lakini imenifanya kufahamiana na watu wengi wa mpira.

“Watu hao wamekuwa na faida kwangu, mawazo yao yanaendana na yangu, nadhani naweza kupiga hatua ndani ya msimu michache ijayo,” alisema kipa huyo.

Akizungumzia soka la Burundi huku akilinganisha na Tanzania, alisema, “Mpira wa nyumbani hasa Bara upo juu.”

Advertisement

 

Advertisement