Kingwendu afurahia sakata la Morrison

Muktasari:

Kinachompa raha mchekesaji nchini, Rashid Mwishehe 'Kingwendu ni vita iliopo kati ya Simba na Yanga, juu ya sakata la winga wa kimataifa, Benard Morrison.

MSANII wa vichekesho nchini, Rashid Mwinshehe 'Kingwendu' amefurahia filamu inayoendelea kati ya Simba na Yanga, kuhusiana na winga wa kigeni Benard Morrison kwamba yanachangamsha mitandao ya kijamii.

Kinachomchekesha Kingwendu ni povu la mashabiki wanaoonyesheana ubabe, wakiwa hawana uhakika kwamba picha litaishaje, juu ya mchezaji huyo kucheza Simba ama Yanga.

Amesema yeye ni Yanga kindakindaki,jambo lililomfurahisha nikuona timu yake haitaki unyonge nakuamua kupambana, hivyo kama shabiki anapata taswira kuona msimu ujao, taji la Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), litakwenda Jangwani.

"Ujue tulikuwa wanyonge sana kipindi cha ugonjwa wa covid 19, tuliona kama tupo kwenye fumbo fulani hivi, mitandao ya kijamii iliandika vitu vilivyotutia wasiwasi, lakini kwa sasa tumepata vitu vinavyotuchangamsha akili,"

"Ukipita kwenye mitandao ya kijamii, utaona kulivyo kwa moto, wakati Simba inatangaza imemsajili Morrison, mashabiki wa Yanga walitikiswa kama sakata halijamalizika, Simba nayo imetikiswa kwa Senzo Mazingisa yaani ni raha juu ya raha,"amesema.

Amesema Simba na Yanga ziendelee kuwepo ili kuendelea kuwapa raha mashabiki wao, kutokana na vituko vinavyofanywa na klabu hizo.

"Ujue unapocheka ndipo unaongeza siku za kuishi, ndani ya wiki hili kuna furaha na huzuni ndio maisha,"akimaliza kwa kicheko akisubiri namna litakavyoisha picha la Morrison.

Sakata la Morrison linaendelea kusikilizwa katika Kamati ya Sheria, Haki na Hadhi za Wachezaji iliyo chini ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambapo leo Jumanne Agosti 12, 2020 wanatarajia kutoa hukumu.

Sakata hilo la kimkataba linahusishwa na ufojaji wa saini ya Morrison kwenye mkataba unaodaiwa aliongeza Yanga ambapo Simba nao wametangaza kumsajili nyota huyo.