Kindoki awakataa Makambo, Kagere

Muktasari:

Kasi ya mastraika hawa wa kigeni kwenye kupasia nyavuni ndio imekuwa ikiwatisha mashabiki, lakini kipa wa Yanga, Mkongomani Nkizi Kindoki wala hawapi nafasi na amewatioa kabisa kwenye ramani ya kutwaa tuzo hiyo.

 Ligi Kuu Bara inaendelea mzunguko wa pili, lakini vita kubwa iko kwenye kusaka kiatu cha dhahabu kwa wafungaji bora, lakini midomoni mwa mashabiki wa soka kuna jina la Heritier Makambo (Yanga) na Meddie Kagere (Simba).
Kasi ya mastraika hawa wa kigeni kwenye kupasia nyavuni ndio imekuwa ikiwatisha mashabiki, lakini kipa wa Yanga, Mkongomani Nkizi Kindoki wala hawapi nafasi na amewatioa kabisa kwenye ramani ya kutwaa tuzo hiyo.
Makambo na Kagere wamefunga magoli 12 kila mmoja, lakini Kindoki humwambii kitu kwa Salim Aiyee (Mwadui), John Bocco, Emmanuel Okwi (Simba) na nyota wa zamani wa Mbeya City, Eliud Ambokile akidai jamaa hao wanajua kufunga bwana.
Alisema anashangaa kuona mashabiki wakishoboka kwa Kagere na Makambo kwa kuwaona kuwa, ndio habari ya mjini wakati kuna mafundi wa maana wanaojua kufunga.
Kindoki aliliambia Mwanaspoti kuwa hadi sasa anaamini nyota, ambaye anaweza kutwaa kiatu hicho ni Aiyee anayepachika magoli 15.
"Tangu nimefika naweza kusema namkubali mchezaji kutoka Mbeya, ambaye nasikia yupo nje ya nchi kucheza soka la kulipwa anaitwa Ambokile ni mpambanaji na hakati tamaa na Aiyee, huyu anajua kucheka na nyavu na naamini ndiye atakayeibuka mfungaji bora,"
"Mchezaji anacheza timu ambayo haina mashabiki wengi anajua nadhani hajafuatiliwa kina Makambo na Kagere wanavuma kwa sababu wanabebwa na mashabiki wao," alisema.
Kindoki alisema wachezaji wengi wazuri wapo katika klabu ndogo ambazo hazina mashabiki wengi wanashindwa kuonekana na majina ya nyota kutoka Simba na Yanga ndiyo yamekuwa yakitawala bila ya kuwa na ufundi mkubwa miguuni mwao.
Alisema kuna baadhi ya wachezaji wamekuwa wakila mishahara mikubwa kutoka klabu zao, lakini hawaonyeshi uwezo mkubwa uwanjani na kumtolea mfano Kagere kuwa nyota huyo alisajiliwa kwa mashindano ya kimataifa, lakini anashindwa kuibeba timu hiyo kutokana na kutoa mchango mdogo tofauti na walivyokuwa wanamtegemea.