Kindoki: Muda ukifika nitasepa Yanga

Muktasari:

Kindoki ambaye alikuwa akihusishwa kutemwa katika kikosi hicho anasema kama aliweza kutua Yanga ambayo ina historia kubwa kwenye soka la Afrika basi uwezo wa kutoka na kwenda sehemu nyingine anao na imani hiyo anayo.

KIPA wa Yanga, Klaus Kindoki ameshangazwa na kauli za wadau wa soka wanaoamini kuwa Yanga ndiyo sehemu pekee kwake  anayoweza kucheza soka na si kwinginepo na kuweka wazi kwamba hapo ni njia tu kwani bado ana safari ndefu.
Kindoki ambaye alikuwa akihusishwa kutemwa katika kikosi hicho anasema kama aliweza kutua Yanga ambayo ina historia kubwa kwenye soka la Afrika basi uwezo wa kutoka na kwenda sehemu nyingine anao na imani hiyo anayo.
"Mimi ni mpambanaji, sikatishwi tamaa na watu nadhani kama nilikuwa mtu wa kukata tamaa basi Yanga ningekuwa nimekimbia kwani sikuwa na mwanzo mzuri nilibezwa na kila mtu lakini nilikomaa na sasa naendelea kukomaa, bado naendelea na safari naamini kwamba sijafika, nahitaji kusonga mbele,"anasema ambaye amebakiza mkataba wa mwaka mmoja.
Aliongeza kwamba hata mkataba wake wa miaka miwili akiwa ametumikia mmoja Yanga, kila mwaka ndani ya mkataba una malengo yake kuhakikisha kwamba anafika mbele zaidi kwa kuweka wazi kuwa una kipengele cha kumruhusu kuondoka endapo atapata timu nyingine nje ya nchi.
"Nafasi ya kipa haina kigezo cha umri, kadri muda unavyozidi kwenda ndio ubora wa walinda milango unaongezeka hivyo naamini bado nina nafasi ya kupambana kusaka timu nyingine, ni miaka sahihi kwangu kwasababu naamini kadri muda unavyokwenda naendelea kuwa bora," anasema Kindoki.