JICHO LA MWEWE: Kinachofuata baada ya Mnyama kumtafuna adui wa kwanza

Muktasari:

  • Kwa JS Saoura niliyoina juzi Jumamosi bado watatu hawa wangeanza kwa pamoja na Simba ingeshinda mechi yake kama kawaida. Hata hivyo, sio kitu kibaya kumsoma adui yako usiyemuelewa vema. Ni kitu kizuri kujaza viungo kwanza.

MABAO mawili ya Meddie Kagere na moja la Emmanuel Okwi yalitosha kuhakikisha Simba inaanza kwa mkwara katika ligi ya wakubwa. Sijui kwanini kocha wa Simba aliamua kumuacha nje Kagere. Nadhani aliwahofia zaidi JS Saoura akaamua kujaza viungo wengi katikati na kuachana na ile kombinesheni yake ya John Bocco, Okwi na Kagere.

Kwa JS Saoura niliyoina juzi Jumamosi bado watatu hawa wangeanza kwa pamoja na Simba ingeshinda mechi yake kama kawaida. Hata hivyo, sio kitu kibaya kumsoma adui yako usiyemuelewa vema. Ni kitu kizuri kujaza viungo kwanza.

Vyovyote ilivyo, mpaka mechi za raundi ya pili zitakapochezwa kwa sasa Simba anaongoza katika kundi lake. Utake usitake. Al Ahly alimchapa AS Vita mabao 2-0 pale Alexandria Misri na hivyo Al Ahly ambao ni kama Real Madrid ya Afrika inashika nafasi ya pili nyuma ya Mnyama wa Msimbazi kwa tofauti ya mabao.

Ni mpaka itakapokwenda Kinshasa katika tarehe ngumu za Januari hii, Simba itakuwa inaongoza kundi. Kwa nilivyoitazama mechi ya juzi, Simba itaanza michuano hii Kinshasa. Mechi ya juzi ilikuwa kama vile Simba imeletewa supu kabla ya chakula.

Achilia ukweli kwamba Simba ilikuwa katika ubora wake, pasi wao, muunganiko wao wa kitimu, ulinzi wao, umaliziaji wao, ubora katika kila eneo, lakini nina mashaka na ubora wa wapinzani wao, JS Saoura. Wamegawa pointi kwa Simba juzi pale Taifa lakini wanaweza kugawa na kwa wakubwa wengine, AS Vita na Al Ahly.

Kinachofuata baada ya ushindi wa Simba juzi ni kusahau haraka matokeo yale. Sawa, ni ushindi mkubwa lakini ukitazama mechi ya Vita na Al Ahly iliyochezwa juzi usiku baada ya mechi ya Simba ni wazi kwamba Vita na Al Ahly zinaweza kumpiga Saoura nyumbani na ugenini.

Mechi ijayo itakuwa kati ya Saoura na Al Ahly pale Algeria na naweza kuona Al Ahly akichukua pointi zote tatu za Saoura ugenini. Huu hautakuwa msaada mkubwa kwa Simba. Na baada ya hapo Vita anaweza kuchukua pointi tatu kwa Saoura.

Kinachotakiwa kwa Simba ni kufanya mambo mawili. Kwanza ni kuhakikisha inashinda mechi dhidi ya Saoura pale ugenini Algeria. Ihakikishe inachukua pointi sita kutoka kwa timu hii ambayo haionyeshi uhai wa kuwasaidia kuwazuia wakubwa siku za mbele.

Baada ya hapo Simba inabidi ianze kuweka mbinu kwa wakubwa. Kwanza ni kuhakikisha walau wanapata sare katika mechi inayofuata pale Kinshasa dhidi ya Vita.

Ikifanua hivyo, itakuwa imejiongezea pointi huku ikiizuia Vita kushinda katika mechi mbili za mwanzo.

Kama itaweza kushinda dhidi ya Vita Jijini Dar es Salaam halafu ikafungwa hata mechi zote mbili dhidi ya Al Ahly, Simba inaweza kumaliza kundi ikiwa na pointi 10.

Ni ngumu kutofuzu hatua inayofuata huku ukiwa na pointi 10 mkononi.

Matokeo ya juzi yameniacha nikiwa siamini kama JS Saoura ianaweza kuifanyia kazi Simba katika siku za usoni. Katika michuano kama hii unahitaji kibonde acharuke na kukusaidia kazi mbele ya safari. Saoura imeniachia maswali mengi kuliko majibu.

Ni kweli ni Waarabu lakini timu yao imeanzishwa mwaka 2008 na inaonekana kuwa katika mchakato wa kuwa klabu kubwa. Sitashangazwa kuona baada ya mechi ya juzi ikiwatamani baadhi ya wachezaji wa Simba.

Ilionekana haijakomaa katika mechi za kimataifa. Mbaya zaidi ipo katika kundi ambalo kuna vigogo waliofika fainali hizi za Afrika miaka ya karibuni, Vita na Al Ahly. Simba inaweza kufanya kazi nzuri katika michuano hii lakini ikaangushwa na JS Saoura kushindwa kuifanyia kazi.

Madhara mengine ambayo Simba itakutana nayo baada ya mechi hii ya juzi ni namna ambavyo wakubwa wataikamia Simba kwa kiasi kikubwa. Mpira wa Afrika umebadilika na sidhani kama Wamisri pamoja na Wacongo wataichukulia Simba kama ambavyo walikuwa wanaichukulia kabla ya kuanza kwa michuano hii.

Kwa sasa watakuwa wanasaka mkanda wa mechi ya mechi ya juzi na kuufanyia kazi kwa kiasi kikubwa. Simba itakuwa katika wakati mgumu katika mechi mbili zinazofuata lakini huu ndio uanaume wa michuano hii kwa jumla.

Mwisho kabisa hongera nyingi kwa Simba kwa kuutendea haki uwanja wake wa nyumbani katika mechi dhidi ya timu ambayo kwa sasa naamini itakuwa vibonde wa kundi, Saoura.

Ilikuwa mechi mwafaka kuanza nayo. Kama ingeanza na Al Ahly nyumbani kisha kufungwa hapana shaka morali ya timu ingepotea na kila kitu kingeharibika.

Lakini juzi Jumamosi ilikuwa mechi sahihi ya kuzidi kutengeneza morali katika timu baada ya kuipika morali hii kupitia kwa Mbabane na Nkana Red Devils.

Wachezaji na mashabiki wataamini kwamba uwanja wao wa nyumbani ni mgumu. Na ndivyo inavyopaswa kuwa katika aina hii ya michuano.