Kina Manula wampa kiburi beki

Friday July 19 2019

 

By Thomas Ng'itu

SIMBA imeimarisha safu yake ya ulinzi kwa kunyakua mabeki kadhaa wakiwamo Wabrazili na jembe moja la maana kutoka Singida United, Kennedy Juma, lakini beki mkongwe Pascal Wawa amewaangalia makipa wa timu hiyo na kujikuta akitabasamu kwa furaha.

Kennedy na wenzake, Tairone Santos na Gerson Vieira wanaungana na kina Wawa, Erasto Nyoni na wengine kuujenga ukuta mgumu wa timu hiyo na hilo limempa fuaraha, lakini uwepo kwa kina Aishi Manula na Beno Kakolanya umemfanya Wawa apate kiburi akiamini mashabiki wa Simba watafurahi msimu ujao.

Wawa alisema makipa hao wawili wote ni bora na ndio wanaowapa morali ya kufanya vizuri katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na mashindano mengine kwani hata mmoja akipatwa na tatizo mwingine atakuwa na uwezo wa kufanya kazi ile ile kwa ufanisi.

Akizungumzia changamoto ya namba kwa msimu ujao, alisema hilo haliweki kichwani kwake kwani anaamini katika kujituma na kufanya kile ambacho anaelekezwa na mwalimu. “Sihofii kuhusu kucheza nadhani hilo ni suala la kocha kuangalia nani anafaa na nani anatakiwa aanzie nje, binafsi najifua ili kuwa fiti muda wote niwapo na timu,” alisema.

Advertisement