Kimenukana manzee, Kahata aigura Gor Mahia

Muktasari:

  • Mkataba wa Kahata na Gor unamalizika mwishoni mwa mwezi huu na taarifa zinaarifu kwamba huenda akaibukia katika klabu ya Yanga SC ya bongo.

Nairobi. Kiungo fundi wa Harambee Stars, Francis Kahata katangaza rasmia kuikacha klabu yake ya Gor Mahia huku akiaga kwa kusema anaamini, mchango wake uliwafaa mno.

Mkataba wa Kahata na Gor unamalizika mwishoni mwa mwezi huu na taarifa zinaarifu kwamba huenda akaibukia katika klabu ya Yanga SC ya bongo.

“Naamini nimeifanyia Gor kazi kubwa na ya kuridhisha tangu nilipojiunga nao nikitokea Thika (United). Kwa miaka yote hiyo mitatu niliyokuwa nayo tumeweza kushinda mataji matatu ya ligi kuu tena kwa mfululizo.

 Hata nikiondoka bado nimekiacha nyuma kikosi dhabiti kinachoweza kutetea ubingwa wa ligi kuu tena na kufanya vyema katika mashindano ya CAF” Alisema Kahata.

Ukiachana na Yanga, pia watani wao wa tangu jadi Simba SC ambayo kwa sasa ipo chini ya uangalizi wa bilionea Mohammed Dewji imeripotiwa kuwa inammezea mate.

Mapema kwenye msimu uliopita, nusura ajiunge na klabu ya Algeria CS Constantine lakini dili hiyo ikagonga mwamba dakika za mwisho.

Mpaka sasa bado haijabainika wazi wazi ni wapi atakapokwenda huku akisema atafanya uamuzi huo baada ya michuano ya dimba la AFCON 2019.