Kimbuga Neymar, Mbappe chatikisa Ligi Kuu England

Thursday June 27 2019

 

London, England. Nyota Eden Hazard ameshaondoka zake. Msimu unaokuja hatakuwapo kwenye Ligi Kuu England tena. Paul Pogba na Romelu Lukaku nao wanapiga hesabu za kuipiga kibuti ligi hiyo baada ya kuwapo kwa taarifa kwamba wawili hao wapo kwenye mikakati ya kuachana na Manchester United.

Christian Eriksen naye yupo njiani kuachana na Tottenham Hotspur, huku mastaa Alexandre Lacazette na Pierre-Emerick Aubameyang wamekuwa kwenye maneno maneno ya kuachana na Arsenal kama si dirisha hili la majira ya kiangazi bas lile la mwakani.

Supastaa Mohamed Salah ameshaweka wazi kwamba huenda msimu utakaoanza utakuwa wa mwisho kwake kuitumikia Liverpool huku jambo kama hilo likitarajiwa kutokea kwa mkali mwenzake wa huko Anfield, Sadio Mane. Hivyo hivyo mastaa wa maana wanavyotarajia kuachana na Ligi Kuu England kwenye kipindi hiki cha uhamisho.

Lakini, wasiwasi zaidi unakuja kutokana na ukweli ni kwamba hata mastaa wa ligi nyingine waliotazamiwa kuja kwenye Ligi Kuu England wanawaza kwenda kwenye timu nyingine za huko Italia, Hispania na Ufaransa.

 Mastaa Neymar, Antoine Griezmann, Kylian Mbappe na Paulo Dybala wote hawatajwi kuwa na mpango wa kwenda kukipiga kwenye Ligi Kuu England.

Akili ya mastaa hao kwa sasa ni kwenda kwenye klabu za huko Hispania kama si Barcelona basi ni Real Madrid, huku Paris Saint-Germain na Juventus nazo zikiwa na mvuto mkubwa kwa mastaa wenye majina makubwa kuliko timu za Ligi Kuu England, wakiwamo vigogo Manchester United, Manchester City, Arsenal, Chelsea, Tottenham na Liverpool.

Advertisement

Baada ya timu za England kutamba kwenye soka la Ulaya kwa msimu uliopita, kwa maana ya michuano ya Europa League na Ligi ya Mabingwa Ulaya, wababe wa Hispania Real Madrid na Barcelona zimeamua kumeza mate ya akili ikiwa pamoja na kufanya usajili wa maana ili kuwa na vikosi vya kutisha msimu ujao.

Juventus nao wamekuwa wakiimarisha wakiwanasa mastaa wa nguvu, akiwamo Aaron Ramsey aliyetoka Arsenal moja ya wababe kwenye Ligi Kuu England.

Kwa hali ilivyo, ndani ya miaka mitatu ijayo kwa maana ya kuanzia sasa, Ligi Kuu England itakuwa kwenye hatari ya kuondokewa na mastaa wake wote wa maana kutokana na ukweli kwamba wakali wake wa sasa wanaoipa hadhi ligi hiyo kama vile Pogba, Mo Salah, Mane, Lukaku, Eriksen na hata Harry Kane wanaweza kushawishika kuachana na ligi hiyo wakati vigogo Real Madrid au Barcelona zitakapohitaji saini zao.

Ilikuwa rahisi sana kwa Barca kunasa huduma ya Philippe Coutinho, Januari mwaka jana na ilikuwa rahisi kwa Real Madrid ilipowang'oa Hazard na Thibaut Courtois kwenye Ligi Kuu England, kama ilivyotaka kumng'oa pia Pogba na Eriksen.

Barcelona wanapiga hesabu za kumnasa Victor Lindelof kutoka Man United kitu ambacho kinazidi kuivuruga zaidi Ligi Kuu England katika miaka ya karibuni.

Wakati wote wa Ligi Kuu England wanasakwa na Real Madrid, Barcelona, PSG na Juventus na kinachoonekana ni kwamba timu hizo zitakwenda kugawana mastaa hao kutokana na nguvu yao ya kifedha na mikakati ya kujijenga kwa mipango ya kutamba kwenye mchezo huo huko Ulaya na duniani.

Hakuna dalili pia ya kumwona Neymar, Mbappe au Griezmann kutua kwenye Ligi Kuu England na hivyo kutishia usalama wa mastaa zaidi kwenda kucheza ligi hiyo licha ya kwamba imekuwa ikisifika kwa kutoa mishahara mitamu.

 

Advertisement