Kilio hiki cha makocha kisipuuzwe

Muktasari:

Naye Kocha Patrick Aussems alipositishiwa mkataba wake na mabosi wa klabu ya Simba, amezungumza matatizo yale yale ambayo Zahera na makocha wengine waliowahi kupita klabu hizo na hata wakati mwingine Azam wamekuwa wakilalamika kuhusu ya kuingiliwa katika kazi yao hasa kufanyiwa usajili na hata kupangiwa vikosi.

WAKATI Kocha Mwinyi Zahera alipotangazwa kutemwa na Yanga mapema mwezi uliopita alikaririwa kwenye vyombo tofauti vya habari akifunguka mambo mengi ambayo aliyavumulia ndani ya Yanga na kulalama namna ambavyo viongozi walikuwa wakimuingilia katika majukumu yake ya kazi.

Alieleza namna ambavyo usajili uliofanyika Jangwani kwamba asilimia kubwa ya wachezaji waliosajiliwa hawakuwa chaguo lake isipokuwa ulifanywa na viongozi naye kujulishwa tu, bila ya mapendekezo yake na mengineyo.

Naye Kocha Patrick Aussems alipositishiwa mkataba wake na mabosi wa klabu ya Simba, amezungumza matatizo yale yale ambayo Zahera na makocha wengine waliowahi kupita klabu hizo na hata wakati mwingine Azam wamekuwa wakilalamika kuhusu ya kuingiliwa katika kazi yao hasa kufanyiwa usajili na hata kupangiwa vikosi.

Aussems anafichua wazi hakupendekeza kuachwa kwa kina Emmanuel Okwi, James Kotei na wengine, pia hakuhusika na usajili wa Wabrazili watatu waliopo sasa Msimbazi kwa vile mchezaji aliyemtaka na kupendekeza wa kigeni ni Francis Kahata pekee.

Inawezekana kabisa, anachokisema Aussems kisiwe na mantiki kwa sasa kwa vile alipaswa kukisema mapema akiwa Simba badala ya kusubiri alipotimuliwa. Ni sawa na alivyopuuzwa Kocha Zahera na Wanayanga kwa vile ilionekana kama ni hasira za kutemwa kwake.

Hata hivyo, bado haya malalamiko ya makocha wanaotemwa ama kuondoka Simba na Yanga na klabu nyingine sio ya kuupuzwa. Inawezekana jambo hilo linalochukuliwa la kawaida au kudhaniwa wanachokizungumza makocha inatokana na hasira za kutemeshwa vibarua vyao, lakini ni lazima malalamiko haya yafanyiwe kazi. Kwani sio mara ya kwanza kutolewa na makocha.

Hawajaanza Zahera ama Aussems. Ni mara nyingi jambo hilo limetokea. Hata Kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ aliwahi kulalama juu ya hilo.

Hii inachochoea uvumi wa miaka mingi kwamba ndani ya baadhi ya klabu, hasa hizi kubwa, kuna matatizo ya viongozi kuvuka mipaka ya kazi zao na kujivika majukumu yasiyokuwa yao kwa masilahi binafsi ama ushabiki na pengine kujigeuza kuwa makocha.

Makocha wote waliotoa lawama hizo sio watoto wadogo, hata kama viongozi wanajaribu kutumia nguvu kubwa kujisafisha na kujibu mapigo kwa kuwashambulia makocha hao, bado ni lazima wenyewe wajitathmini na kujipima kwa sababu hata mashabiki na wanachama wanaujua ukweli.

Wanafahamu viongozi ndani ya klabu moja wamekuwa wakigawana majukumu ya usajili wakati mwingine kwa utashi na ushabiki badala ya mahitaji ya timu ama hitaji la benchi la ufundi, ndio maana unaweza kukuta timu inahitaji kiungo mkabaji ama beki wa kati, lakini wakasajiliwa mastraika ama kipa bila sababu za maana!

Hata kwenye upangwaji wa timu kuna tuhuma wakati mwingine, unakuta viongozi wanakuwa na listi zao tofauti na kile kinachohitajika kulingana na ufanisi na ufiti wa wachezaji mazoezini na hata aina ya mchezo wanaokabiliana nao kimbinu.

Ndio maana, tunawakumbusha viongozi na hata wanachama na mashabiki wa klabu husika kujitathmini na kutambua kuwa, kama hakutakuwa na badiliko katika hili, basi daima hii ingia-toka ya makocha itadumu milele.