Kilichomrejesha Ninja Tanzania hiki hapa!

Muktasari:

Kuonekana kwake akifanya mazoezi na Yanga, klabu yake ya zamani, kumezua maswali kwa mashabiki wakihoji ameshindwa kupambana na kutumia fursa aliyoipata kwenda nje?

BEKI Abdallah Shaibu ‘Ninja’ hakutaka kufa na tai shingoni kwa kisingizio cha kuonekana anacheza Ulaya. Alipoona maisha yanaenda kombo huko, akaona mkataa kwao ni mtumwa, akarejea Tanzania.

Kuonekana kwake akifanya mazoezi na Yanga, klabu yake ya zamani, kumezua maswali kwa mashabiki wakihoji ameshindwa kupambana na kutumia fursa aliyoipata kwenda nje?

Mwanaspoti limefanya mahojiano na Ninja ili aeleze kwa nini amerejea Tanzania, je amevunja mkataba na timu ya labu yake ya Jamhuri ya Czech ya MFK Vyaskov? Malengo yake ni yapi?

Beki huyo wa kati anafunguka mazito namna ambavyo alikuwa anaishi maisha magumu ya kuungaunga, huku akishindwa kutoa msaada katika familia yake inayomtegemea.

“Kwenda kwangu nje mama yangu alikosa msaada kwa watu, wakati ameingiliwa na mafuriko, wanamwambia mwanao anacheza soka la kulipwa, ujue hii inaumiza. Baba yetu alifariki hivyo namtunza mama yangu, nikiangalia sina jambo halafu najikaza kisabuni, nikaona yote hayo ya nini,” anasema.

AMEVUNJA MKATABA

Anasema amevunja mkataba wake na MFK Vyaskov Mei mosi, na anataja sababu kuwa ni timu hiyo kushindwa kumlipa stahiki zake na kumfanya kuishi maisha magumu Ulaya.

Anasema kilichotokea kwamba baada ya kusaini mkataba wa miaka minne na MFK Vyaskov, alipelekwa kwa mkopo wa miezi minne katika klabu ya LA Galaxy ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS).

Baadaye akarejea Tanzania ambapo akaambiwa kuna dili la Ulaya ambalo halikuwa la kusaini moja kwa moja mpaka apitie katika klabu ya Rigas Football Skola ya Ligi Kuu ya Latvia.

“Ipo hivi baada ya kutoka Marekani katika timu ya LA Galaxy, niliambiwa nisaini katika klabu ya Rigas Football Skola kama njia ya kwenda kwenye timu nzuri zaidi za Ulaya ambako sikuambiwa ni timu gani nitakwenda kucheza, nikafanya hivyo. Lakini baadaye ikawa tofauti na makubaliano yetu.”

Anaongeza: “Kwanza kabla sijaenda kwenye hiyo timu, nikawa sipewi mshahara, nikajipa uvumilivu nikidhani baada ya kujiunga nao kila kitu kitakaa sawa, nikaona mambo yanaenda vilevile,” anasema.

Anasema alikuwa akiwasumbua sana kudai mshahara wake. Walikuwa wanampa Dola 250 (sawa na Shilingi 500,000), kitu kilichokuwa kinampa ugumu ugenini na kufanya maisha kuwa magumu.

“Ilifikia hatua kula wakati mwingine nilikuwa najibana, zipo siku ambazo ilikuwa inatokea napiga ndefu (nashinda bila ya kula), ukiachana na hilo nategemewa na familia, hivyo kukaa kwangu nje wanaona kama napata wakati nina hali ngumu.

“Kuna siku mama yangu nyumba iliingia maji kipindi cha ugonjwa wa covid 19, nikamtumia meneja wangu video ili anisaidie pesa ya kumhamisha, akakaa kimya, ninasomesha mdogo wangu anasoma chuo, akarudishwa ada, nikamwambia akakaa kimya, nikawaza kwa nini nijiumize na kuonekana kwa watu nipo nje wakati napoteza muda?”

Anasema baada ya kuona mambo yanazidi kuwa magumu akamtaarifu meneja wake anavunja mkataba, akamtaka kuwa mvumilivu, huku akiendelea kumtafutia madili mengine, lakini alishindwa kutokana na kuishi ugenini bila ishu.

ALICHOJIFUNZA

Anasema kitendo cha kutoka kwenda klabu ya LA Galaxy na Rigas Football Skola, hakijamuacha bure amejifunza kuamini katika kitu anachokifanya bila kujali watu wanaona nini juu yake.

“Ni kweli sijanufaika na chochote nilivyoenda Rigas Football Skola, tofauti na LA Galaxy ambako angalau nilifanya maendeleo nje na uwanjani, lakini nikizungumzia kiufundi nimepata madini mengi,” anasema.

KWA NINI KARUDI?

“Najisemea mimi maisha niliyoishi nje, nisingeweza kung’ang’ania kukaa huko wakati silipwi, halafu sioni kama panamwanga wa kucheza, hivyo nimeona nina muda mwingine wa kujipanga nikiwa nyumbani kuliko kufeki maisha,” anasema.

AMESAINI YANGA?

Alipoulizwa ipo ishu anayohusishwa na kusaini Yanga? Ninja alijibu, amefanya mazungumzo na timu hiyo, imeonyesha nia ya kumrejesha lakini bado hajasaini mkataba nao.

“Ni kweli nimefanya mazungumzo nao kwa kirefu, maana kwa sasa mimi nipo huru, ila kusaini bado, hivyo tukifikia mwafaka nitakuwa wazi kusema na kama dili litafeli basi nitasaini popote penye maslahi na mimi, maana soka ni kazi inayofanya familia yangu inategemee,” anasema.

Alipoulizwa anaionaje nafasi yake Yanga, alisema: “Naheshimu wachezaji waliopo, lakini mimi nimejifunza mbinu tofauti huko nilikotoka na kurejea kwangu haina maana kwamba sina uwezo.”

HANA MENEJA

Anasema kwa sasa hana meneja, isipokuwa kuna mtu yupo Zambia ambaye anamtafutia timu za nje. “Huyo mtu anapenda ninavyocheza, alinipigia simu kuniunganisha na timu mbalimbali za nje.”

WASHKAJI GALAXY

Anasema baada ya kucheza LA Galaxy ya Marekani kwa mkopo, amejenga urafiki na wachezaji wa timu hiyo, ambao wanaendelea kumpa ushauri namna ya kusimamia kipaji chake kufika mbali.

“Wenzetu wanaamini wakiwa hai na afya njema basi wanaweza wakatimiza ndoto zao, baada ya kuwaambia nimerudi nyumbani, wananiambia jipange, usikatishwe tamaa na jua unachokihitaji,” anasema.

CHANGAMOTO

Anasema katika timu hizo mbili, amekutana na utamaduni ambao hauendani na Tanzania kama lugha ambayo alikuwa anapambana kuhakikisha anaelewana na wenzake.

“Mfano huko nilikotoka unakuta chakula chao wanaleta chipsi na kipande cha kuku hiyo ndio imeisha, najikuta sishibi hivyo nilikuwa natafuta namna ya kufanya niishi.

“Kiukweli Ulaya sijaambulia hata kununua nguo ya kumbukumbu. Nilizotoka nazo Marekani ndizo nilizorudi nazo, ila imenikomaza kiakili,” anasema.

Ninja alipata dili la kusaini MFK Vyaskov akitokea Yanga, aliyoichezea misimu miwili 2017/18 akitokea Taifa Jang’ombe, Zanzibar.