Kili Stars kazi imeanza Kampala

Muktasari:

Mara ya mwisho kwa Kilimanjaro Stars kutwaa ubingwa wa mashindano ya Chalenji ilikuwa ni mwaka 2010.

Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' leo kitafanya mazoezi ya kwanza tangu kilipowasili jijini Kampala jana tayari kwa ushiriki wake katika mashindano ya Chalenji.
Mashindano hayo yanaanza kesho yakishirikisha nchi tisa (9) wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ambao ndio waandaaji na wasimamizi.
Mazoezi hayo ya Stars leo ambayo yataanza kuanzia saa 10 jioni, yatafanyika katika viwanja vya Kawempe vilivyopo umbali wa Kilomita tano (5) kutoka katika hoteli ya Sojovalo ambako msafara wa Stars umehamia kutoka ile ya G One ambayo ilifikia jana jioni.
Kocha mkuu wa Kilimanjaro Stars, Juma Mgunda alisema kuwa mazoezi hayo yatalenga zaidi kuweka sawa miili na mbinu kadhaa.
"Tunamshukuru Mungu kwamba wachezaji wote wako sawa na wazima wa afya. Hamasa na molali ya vijana iko juu na kikubwa ni kwamba tuna imani tutafanya vizuri," alisema Mgunda