Kili Queens, Uganda vita isiyoumiza Cecafa wanawake

Muktasari:

Kilimanjaro Queens imepania kufanya kweli kwenye mchezo huo ambapo Kocha Bakari Shime 'Mchawi Mweusi' amewatoa wasiwasi Watanzania kuwa watashinda.

NUSU fainali ya michuano ya Cecafa wanawake, inaendelea leo Jumamosi, wenyeji Tanzania Bara 'Kilimanjaro Queens' watakipiga na Uganda wakati Kenya wataonyeshana ubabe na Burundi.

Kilimanjaro Queens ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo ambayo mwaka huu imeshirikisha timu za mataifa nane kutoka Afrika Mashariki na Kati.

Watacheza na Uganda jioni ya leo Jumamosi saa 10:00 baada ya mechi ya Burundi na Kenya itakayopigwa saa 7:45 mchana na michezo yote inapigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Kilimanjaro Queens imepania kufanya kweli kwenye mchezo huo ambapo Kocha Bakari Shime 'Mchawi Mweusi' amewatoa wasiwasi Watanzania kuwa watashinda.

"Moto ni ule ule, timu iko vizuri zaidi ya tulivyoanza mashindano na hata wale wachezaji muhimu tuliokuwa tumewakosa mechi zilizopita kwa sababu mbalimbali wamerudi, "alisema Shime.

Aliwataja wachezaji hao ni Stumai Abdallah alikuwa majeruhi, Opa Clement, Happness Mwaipaya aliowapumzisha na Julitha Singano alikuwa na kadi mbili za njano wanarudi kwenye timu.

Kocha wa Uganda, Faridah Bulega alisema: "Tumejiandaa vizuri kuona namna gani tunashinda mchezo wetu Kilimanjaro Queens tunajua tunacheza na timu nzuri na sisi ni wazuri pia."

Mataifa hayo manane kutoka Afrika Mashariki na Kati mbali na Kilimanjaro Queens, Uganda, Kenya na Burundi, walikuwepo Djibouti, Ethiopia, Sudan Kusini na Zanzibar waioaga hatua ya makundi.

Kilimanjaro Queens walichukua ubingwa mfululizo mwaka 2016 na 2018 yalipofanyika Burundi,  Zanzibar imechukua mara moja 1986 na baada ya hapo yalisimama kama miaka 30.