Kili Marathon imenoga kinoma huko

Muktasari:

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli alisema kuwa Kili Canvas itawekwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na baadaye mjini Moshi ili kuwahamasisha wakimbiaji mbalimbali kuelekea kilele cha Kili Marathon.

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) imezindua Kili Canvas itakayotumika kuhamasisha wakimbiaji wa vitongoji tofauti vya Jiji la Dar es Salaam na mji wa Moshi katika kuelekea kilele cha mbio za Kili Marathon zinazotarajiwa kufanyika Machi Mosi mkoani Kilimanjaro.

Programu hiyo ya Kili Canvas ni matokeo ya mashindano ya uchoraji ya ‘Jiachie na Kili Canvas Competition 2020’ ambapo washindani walitakiwa kuchora mchoro kwenye kitambaa kigumu (canvas) kuhusiana na mashindano hayo.

Mkazi wa Dar es Salaam, Athumani Hamis aliibuka mshindi katika shindano hilo na kuzawadiwa Sh2 millioni na mchoro wake utatumika wakati wa mashindano ya Machi Mosi.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli alisema kuwa Kili Canvas itawekwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na baadaye mjini Moshi ili kuwahamasisha wakimbiaji mbalimbali kuelekea kilele cha Kili Marathon.

Alifafanua zaidi kuwa kutakuwa na ‘chip’ maalumu ambayo mkimbiaji atatakiwa kuwa nayo wakati akikimbia na atakapopita kwenye canvas atapigwa picha na itatumwa moja kwa moja kwenye simu yake.

“Ili uweze kupigwa picha na kutumiwa kwenye simu yako kwa wale wakimbiaji ni lazima ujisajili na kupewa chip maalumu ambayo utaelekezwa wapi pa kuiweka wakati unakimbia,” alisema Kikuli.

“Mara tu utakapopita karibu na Canvas kamera zetu zitakutambua na kukupiga picha kwa teknolojia maalumu na kutumiwa papo hapo kwenye simu yako.”

Kikuli alivitaja vituo vitakavyowekwa canvas hiyo kuwa ni Masaki, Goba na Temeke kwa Dar es Salaam na baadaye kuhamia Moshi mkoani Kilimanjaro.

Katika hatua nyingine, Kikuli aliwapongeza washiriki wote waliojitokeza kushiriki shindano la ‘Jiachie na Kili Canvas Competition 2020’ lililofanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu, akisifu ubora wa kazi zao.

“Washiriki wote walifanya vizuri, ila mwisho wa siku tukapata mshindi mmoja kutokana na taratibu za shindano lenyewe,” alisema.