Kilimanjaro Stars , Zanzibar Heroes kufa au kupona

Muktasari:

Hata hivyo, hata ikitoka sare, inaweza kusonga mbele iwapo Zanzibar itapoteza au kutoka sare na Kenya na hata ndugu zao hao wakiibuka na ushindi, Stars inaweza kunufaika na kutinga nusu fainali ikiwa tu itamaliza ikiwa na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ inakabiliwa na dakika 90 za presha wakati itakapokabiliana na Sudan leo katika mchezo wa mwisho wa kundi B la mashindano ya Chalenji yanayoendelea jijini Kampala, Uganda.

Aina ya matokeo yanayohitajika kwa kila timu pamoja na takwimu zinazohusu timu hizo, zinatoa picha ya wazi ya ugumu na ushindani mkubwa ambao unaonekana utakuwepo katika mechi hiyo.

Stars ambayo inashika nafasi ya pili katika kundi B nyuma ya Kenya ikiwa na pointi tatu ilizokusanya katika michezo miwili iliyocheza dhidi ya vinara wa kundi hilo na ndugu zao wa Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ inahitajika kupata ushindi tu leo ili itinge nusu fainali.

Hata hivyo, hata ikitoka sare, inaweza kusonga mbele iwapo Zanzibar itapoteza au kutoka sare na Kenya na hata ndugu zao hao wakiibuka na ushindi, Stars inaweza kunufaika na kutinga nusu fainali ikiwa tu itamaliza ikiwa na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Lakini ikiwa itafungwa, Stars itaaga rasmi mashindano hayo kwani itabakia na pointi zake tatu ambazo hazitoweza kufikia zile za Kenya wala Sudan au Zanzibar ikiwa nayo itashinda mchezo wake wa mwisho.

Presha nyingine ya Stars katika mashindano hayo inaweza kuletwa na aina ya matokeo ambayo timu hizo mbili zimekuwa zikiyapata katika mashindano ya Chalenji na mengineyo katika siku za hivi karibuni.

Katika mashindano ya Chalenji, timu hizo zimekuwa na matokeo yanayofanana jambo linaloashiria ugumu wa pambano la leo.

Takwimu za michezo kumi ya mwisho ambayo kila timu imecheza katika mashindano hayo, zinaonyesha Sudan na Kilimanjaro Stars hazipishani sana.

Kila moja imeibuka na ushindi mara tatu, zimetoka sare mara mbili kwa kila timu na timu hizo kila moja, imepoteza mechi tano kati ya hizo 10 za mwisho ambazo wamecheza za mashindano hayo ya Chalenji.

Katika mechi zake hizo 10, Sudan imefunga mabao 12 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 12 pia wakati Kilimanjaro Stars yenyewe imefunga mabao 11 na kuruhusu nyavu zake zitikiswe mara kumi.

Ikiwa Stars itafanikiwa kupata matokeo yatakayoivusha, itakuwa inatinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo kwa mara ya 15 tangu yalipofanyiwa marekebisho ya muundo wake mwaka 1973.

Mara 14 ambazo Kilimanjaro Stars ilitinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Chalenji ni 1975, 1979, 1980, 1981, 1990, 1992, 1994, 2002, 2008, 2009, 2010, 2011, 2012 na 2013

Hata hivyo,hilo limeonekana kutompa shida kocha wa Kilimanjaro Stars, Juma Mgunda ambaye ametamba vijana wake wako tayari kwa mchezo huo.

“Niseme tu nafurahi kuona vijana wangu wote ni wazima na wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo. Katika mechi zilizopita ni kweli kuna udhaifu ambao tumeubaini na tumeshaufanyia kazi.

Hata hivyo, siwezi kuutaja wala kusema mbinu ambazo tutazitumia hapa na badala yake tutakwenda kufanyia kazi uwanjani,” alisema Mgunda.